DE-D AHIMIZA VIKUNDI KUREJESHA MIKOPO KWA WAKATI


Na, Ernest Magashi

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Adelina Mfikwa, amewataka wanufaika wa mikopo isiyo na riba kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu mipango ya vikundi vyao na kurejesha mikopo kwa wakati, ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo.Mfikwa ametoa wito huo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mikopo isiyo na riba kwa vikundi 24 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, iliyofanyika katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.Alisema kuwa mchakato wa utoaji wa mikopo hiyo ulianza mwaka jana na umefanikisha vikundi 24 kunufaika na mikopo hiyo bila riba.Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskasi Muragili, alisema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.“Tumeanza mwaka vizuri na mikopo hii itawasaidia kufikia malengo yenu. Serikali ina matumaini makubwa kupitia mikopo hii,” alisema Muragili.Aliongeza kuwa mikopo hiyo si ya ghafla bali ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Serikali wa kuwawezesha wananchi kiuchumi na kutokomeza umaskini.“Ukirejesha mkopo kwa wakati bila usumbufu, unapata fursa ya mkopo mwingine tena wa kiwango cha juu zaidi,” alisisitiza.

Mhadis Muragili aliwataka wanufaika kuwa na nidhamu ya fedha, akitoa mfano wa wajasiriamali walioanza na mitaji midogo na baadaye kuendesha biashara kubwa, akitaja kampuni ya Lifetime Furniture ya Kahama kama mfano hai wa mafanikio.“Lengo la Serikali ni kuwawezesha wananchi kiuchumi. Hakuna fedha ndogo au kubwa katika safari ya ukuaji wa kiuchumi,” alisema.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, akiwasilisha salamu za Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, aliwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku Serikali ikiendelea kupeleka fedha za miradi ya maendeleo.“Nawatakia heri ya mwaka mpya. Mbunge wetu, Mhe, Dkt. Doto Biteko, amenituma niwajulishe kuwa anawapenda sana, na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anaipenda Bukombe,” alisema Kagoma.

Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano kati ya madiwani na wataalamu wa Halmashauri, lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani limefanikiwa, na kuwasihi wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya maendeleo.Kila kikundi, ikiwemo cha vijana wa bodaboda, hakikisheni mnazitumia fedha hizi kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati, ili ziwanufaishe ninyi na vikundi vingine,” alisema.Aliwasihi wajasiriamali wanawake kutumia mikopo hiyo kwa shughuli za uzalishaji badala ya matumizi yasiyo ya kimaendeleo, akisema,“Kununua khanga hakutakusaidia kurejesha mkopo. Zitumieni fedha hizi kulingana na malengo yenu, na maendeleo yatakuja kupitia kazi na bidii.”Fedha hizo zimetolewa kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi, ambapo shilingi milioni 133 zimetengwa kwa ajili ya vitendea kazi, na kufanya jumla ya fedha zilizotolewa kwa wajasiriamali kufikia shilingi milioni 208.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Bodaboda Sinamila, Faustine Ndambi, aliwataka wanufaika wa mikopo hiyo kuwa waaminifu, waadilifu na mfano bora kwa vijana wengine.“Hii ni mara ya kwanza kwa Kijiji cha Sinamila kupata mkopo wa asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, kama ilivyoelekezwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.Naye Katibu wa Kikundi cha Bodaboda Sinamila, Emmanuel Mussa, aliishukuru Serikali kwa ushirikiano uliotolewa kupitia uongozi wa kata na Halmashauri, akisema kuwa kwa sasa Kata ya Butinzya imejaa fursa nyingi kwa vijana.

Alisisitiza kuwa maendeleo yako karibu iwapo vijana watazitumia ipasavyo fursa zinazotolewa na Serikali.

Comments