BODABODA WAHAMASISHWA KUANZISHA SACCOS

Na, Ernest Magashi

Maafisa usafirishaji kwa pikipiki (bodaboda) Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamehamasishwa kuanzisha umoja wa kifedha (SACCOS) utakaowawezesha kukopeshana, kuondokana na mikopo yenye riba kubwa na kukuza uchumi wao binafsi pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.Wito huo umetolewa leo 4,2026 na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, wakati akisikiliza kero na changamoto za maafisa usafirishaji katika Kata ya Uyovu.Dkt. Biteko alisema kuwa endapo bodaboda wataanzisha SACCOS, kuisajili kisheria na kufungua akaunti ya benki, yupo tayari kuwatafutia mtaji wa shilingi milioni 100 zitakazowawezesha kukopeshana, kwa kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii.“Nawaomba muanzishe SACCOS itakayohudumia bodaboda wa wilaya nzima ili mkopeshane na kukuza mitaji yenu. Nikishuhudia mmejipanga vizuri kisheria,  mtanufaike kwa pamoja na kuinua uchumi wenu,” alisema Dkt. Biteko.Aidha, aliwahimiza vijana kuendelea kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba inayotolewa na halmashauri, akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.“Serikali kila mwaka hutenga fedha kwa ajili ya vijana. Niwaombe muwe na nidhamu ya fedha ili kuboresha maisha yenu. Natamani kuona maisha yenu yanabadilika na kazi yenu inaheshimika, kwa kuwa mnaisaidia jamii na taifa kwa ujumla kwa kuongeza kipato,” aliongeza.Awali, Diwani wa Kata ya Uyovu, Matayo Kagoma, alimshukuru Mbunge kwa kuendelea kuwafikia makundi mbalimbali ya wananchi, hususan vijana, kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.“Mbunge amekuwa na dhamira ya dhati ya kulifikiria kundi hili la bodaboda. Ni jukumu letu vijana kumuunga mkono kwa vitendo kwa kuanzisha SACCOS itakayowasaidia kuinuka kiuchumi,” alisema Kagoma.Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Maafisa Usafirishaji (Bodaboda) Wilaya ya Bukombe, Leonard Mtuta, alisema wilaya ina jumla ya maafisa usafirishaji 1,972 ambao watanufaika na kuanzishwa kwa SACCOS hiyo.

Alisema SACCOS itawasaidia kukopeshana wao kwa wao na kuwaondoa kwenye mikopo yenye riba kubwa ambayo imekuwa kikwazo kikubwa katika kufikia malengo yao ya kiuchumi.

Mtuta alimshukuru Dkt. Biteko kwa kuwajali bodaboda na kuwaomba wenzake kuyatekeleza maelekezo ya kiongozi huyo, ikiwemo kuheshimu na kusimamia kipato chao hata kama ni kidogo, ili kujenga mustakabali bora

Comments