Askofu wa Kanisa la Ufunuo Jimbo la Geita, Rosemary Mashauri Bendera, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo, huku akiwahimiza wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kuijenga na kuendeleza Wilaya ya Bukombe.
Pongezi hizo zilitolewa Jumapili wakati wa ibada ya shukrani kwa Mungu baada ya kuvuka mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka 2026, iliyofanyika katika Kanisa la Ufunuo mjini Ushirombo, wilayani Bukombe.
Katika ibada hiyo, Askofu Rosemary aliwaomba waumini kuendelea kuiombea Serikali na viongozi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Alitaja baadhi ya miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa wilayani humo, ikiwemo ujenzi wa soko la kisasa, stendi ya mabasi na uwanja wa mpira wa miguu, kama vielelezo vya dhamira ya Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, Askofu Rosemary aliwatunuku wachungaji 12 daraja la uchungaji kamili na kuwakabidhi vifaa vya kazi, akiwahimiza kumtumikia Mungu kwa uaminifu kwa kushirikiana na Serikali pamoja na jamii zinazowazunguka katika maeneo watakayopangiwa.
Vilevile, aliwasisitiza wazazi na walezi kuwekeza katika elimu ya watoto wao kwa kuhakikisha watoto waliofikia umri wa kuandikishwa darasa la awali na kidato cha kwanza wanaandikishwa na kuhudhuria shule, sambamba na jitihada za Serikali za kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, katika ziara zake za kikazi hivi karibuni amekuwa akihamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo kwa kuchangia nguvu kazi, hususan katika ujenzi wa zahanati na shule.
Dkt. Biteko amesema Serikali inatarajia kukarabati shule 23 pamoja na miundombinu yake, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za elimu wilayani Bukombe, huku akisisitiza kuwa jukumu la wazazi na walezi ni kuhakikisha watoto wote wanapelekwa shule kwa wakati.

Comments
Post a Comment