AJALI YA BASI NA LORI KUGONGANA USO KWA USO YAUA MTU MMOJA, 12 WAJERUHIWA SHINYANGA


Na, Ernest Magashi

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi la abiria na lori (roli), ajali iliyotokea katika eneo la Mnada wa Tinde, wilayani Shinyanga, mkoani Shinyanga.Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa dereva wa lori la mizigo ndiye aliyefariki dunia papo hapo katika tukio hilo lililotokea saa 12:30 asubuhi, Januari 27, 2026, katika Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.Akizungumza kuhusu chanzo cha ajali hiyo, Kamanda Magomi amesema kuwa basi lilikuwa likiendeshwa kwa mwendokasi, na lilipofika eneo la Mnada wa Tinde liligonga toroli la matikiti, kabla ya kugongana uso kwa uso na lori.

Ameeleza kuwa basi hilo lilikuwa na jumla ya abiria 42, ambapo 12 walijeruhiwa; kati yao watano hali zao ni mbaya na wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza, huku wengine saba wakipatiwa matibabu katika Zahanati ya Tinde.“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi la Kisire ambaye hakuchukua tahadhari zinazohitajika. Baada ya ajali kutokea alikimbia, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili achukuliwe hatua za kisheria,” amesema Kamanda Magomi.Amesema ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya KISIRE lenye namba za usajili T 229 EEL, lililokuwa likisafiri kutoka Kahama kuelekea Mwanza, na lori lenye namba za usajili RAE 849 N, lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea nchini Rwanda, likiwa limebeba shehena ya mchele.

Kwa upande wake, mmoja wa majeruhi, Robert Daudi, amesema alikuwa akisafiri pamoja na watoto wake watatu, na kwamba baada ya kusikia kishindo kikubwa ndipo walitambua kuwa wamepata ajali. Ameongeza kuwa, licha ya abiria wezao kujeruhiwa, yeye na watoto wake wako salama.


Comments