WANANCHI 275 WAFANYIWA UCHUNGUZI WA SARATANI BUKOMBE


Na Ernest MagashiJumla ya wananchi 275 Wilayani Bukombe, mkoani Geita, wamefanyiwa uchunguzi wa saratani katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kupitia Kampeni ya Huduma za Mkoba (Hon. Samia Suluhu Hassan Outreach Services) inayoendeshwa na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Katika uchunguzi huo, wanawake 210 walipimwa saratani ya shingo ya kizazi na matiti, huku wanaume 65 wakifanyiwa uchunguzi wa tezi dume.Kwa mujibu wa taarifa za ORCI Kati ya wanaume 65, wanaume 4 walibainika kuwa na viashiria vya saratani na wameelekezwa kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Kwa upande wa wanawake 210, wanawake 9 walikutwa na mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi na kupatiwa matibabu ya kuzuia saratani kuendelea.Wanawake 2 waligundulika kuwa na uvimbe unaohitaji uchunguzi zaidi.Katika siku ya pili ya kampeni, wataalamu wa ORCI wakiongozwa na Dkt. Maguha Stephane, Meneja wa Huduma za Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma, walifanya kikao na uongozi wa hospitali ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Deograsia Mkapa.

Dkt. Maguha alisema lengo kuu la Huduma za Mkoba ni kubadilishana ujuzi kati ya ORCI na hospitali za wilaya, ili kuboresha mfumo wa utambuzi na rufaa za wagonjwa.

“Serikali ya Awamu ya Sita inatambua changamoto za gharama za matibabu ya saratani, ndiyo sababu matibabu ORCI hutolewa kwa kuzingatia uwezo wa mgonjwa. Hakuna anayefika ORCI na kukosa matibabu. Muhimu ni kufika mapema,” alisema.Kwa upande wake, Dkt. Mkapa alibainisha changamoto ya wagonjwa kushindwa kufika katika vituo vya rufaa kutokana na gharama za usafiri na mazingira ya kijamii.“Wengi wakipewa rufaa kwenda Bugando au ORCI hushindwa kutokana na hali duni kiuchumi.Tunahitaji muongozo wa pamoja ili wananchi wasiachwe nyuma,” alisema.

Mbali na vipimo hospitalini, timu ya ORCI ilifika katika maeneo mbalimbali ya Bukombe ikiwemo Soko la KariakooSoko Kuu la vyakula na nguoStendi ya Ushirombo, maeneo ya mama lishe, na mtaa kwa mtaa kutoa elimu ya saratani.

Balozi wa Saratani Tanzania, Cedou Mandigo maarufu kama “Babu wa Kitaa”, aliendelea kuwahamasisha wananchi kufanya uchunguzi mapema.“Kupimwa na kukutwa na saratani si hukumu ya kifo. Ikigundulika mapema, inatibika. Tusisubiri hadi hali iwe mbaya,” alisema.

Wataalamu wa ORCI, akiwemo Dkt. Maguha Stephane na Dkt. Merry Kondowe wa Global Medicare, walitoa majibu ya kitaalamu kwa wanawake kuhusu manufaa na muda sahihi wa kufanya uchunguzi wa saratani.

ORCI imeahidi kuendelea kutoa huduma za uchunguzi, matibabu, ushauri na rufaa bila gharama kupitia kampeni ya Huduma za Mkoba, ikilenga Kuongeza uelewa Kugundua saratani mapema Kupunguza vifo vinavyotokana na saratani Kuimarisha afya za jamii kwa ujumla. 

Comments