DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Wizara ya Nishati imezindua rasmi Mita Janja za Umeme, hatua inayoelezwa kuwa mwanzo wa mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za umeme nchini. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya uzinduzi huo ilikuwa “Luku Kijanja, Ukilipa Huo.”
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi amesema Mita Janja ni hatua muhimu kwa maendeleo ya shirika hilo na kwa mustakabali wa wateja wake, kwani zitapunguza usumbufu, kuongeza ufanisi na kuimarisha uaminifu wa huduma za umeme nchini.
Amesema mita hizo mpya zitawawezesha wateja kupata taarifa za umeme unaokaribia kuisha kwa wakati, kuingiza umeme popote walipo bila kulazimika kufika nyumbani, pamoja na kuongeza usalama wa matumizi ya umeme kupitia mfumo wa kidigitali.
Waziri Ndejembi amesema TANESCO inahudumia zaidi ya wateja milioni 5.5, hivyo mabadiliko ya mita yatafanyika kwa hatua kulingana na mahitaji ya kila eneo. Ameagiza usambazaji wa mita hizo uharakishwe katika mikoa yote, hususan kwa wateja ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto za mara kwa mara.
Aidha, amelitaka shirika hilo kuanzisha programu maalumu ya simu (app) itakayojumuisha huduma zote za TANESCO ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa, malipo na mawasiliano kwa wateja. Ameongeza kuwa elimu kwa umma inapaswa kutolewa mara kwa mara kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaelewa kwa undani namna ya kutumia mita hizo.
Amesisitiza pia kuwa ni muhimu TANESCO kuendelea kubuni teknolojia mpya zinazoendana na kasi ya dunia ya kisasa:
“Ni lazima shirika mhakikishe mnaendana na kasi ya teknolojia. Haiwezekani TEHAMA ishafika mbali na sisi tukaendelea kutumia mifumo ya zamani,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange amesema Mita Janja zina uwezo wa kutunza kumbukumbu za matumizi ya umeme hadi miezi 13, jambo litakalosaidia kutatua changamoto kama ununuzi wa umeme kimakosa, kutambua tabia za umeme na kuboresha majibu kwa wateja wanaoulizia mwenendo wa matumizi yao.
Twange amesema mita hizo zinaweza kusaidia TANESCO kukata au kurejesha umeme bila kufika eneo la tukio, na hata kuwalenga wahusika maalumu bila kuathiri maeneo mengine. Ameongeza kuwa usalama wa mita umeimarishwa zaidi na iwapo zitaingiliwa, mfumo unaweza kubaini mapema kuliko ilivyokuwa awali.
Amefafanua pia kuwa moja ya faida kubwa kwa wateja ni kwamba umeme unaingia moja kwa moja kwenye mita pindi unaponunuliwa, bila kungoja token au kutumia remote, hali inayomuepusha mteja na usumbufu wa kukosa betri au kuchelewa kwa aliyekuwa akimiliki kifaa hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kati ya wateja zaidi ya milioni 5.5 wa TANESCO, zaidi ya milioni 1.5 wanapatikana Dar es Salaam, hivyo mkoa huo unatarajiwa kuwa kitovu cha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mfumo huo.
Uzinduzi huu umefungua rasmi dira mpya ya kidigitali katika usimamizi na matumizi ya umeme nchini, huku serikali ikiahidi kuendeleza maboresho ya kimfumo na kiteknolojia ili kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto kwa wateja.



Comments
Post a Comment