Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Dkt. Doto Biteko, aanza kazi kwa kushiriki ujenzi wa Zahanat, pia amewashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumuamini tena na kumpa kura nyingi katika uchaguzi, zikiwemo kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Biteko ametoa shukrani hizo leo, Desemba 29, 2025, wakati akishiriki zoezi la ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Butinzya kwa kusongeza zenge pamoja na wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa jamii katika miradi ya maendeleo.
Akizungumza na wananchi, Dkt. Biteko alisema ushindi wao katika uchaguzi ni ushahidi wa imani waliyopewa, na tayari Serikali imeanza kutekeleza ahadi zake kwa kuleta fedha za miradi ya maendeleo ili kuboresha huduma za kijamii.
Aidha, aliwapongeza wananchi wa Butinzya kwa kujitolea kwa nguvu zao katika ujenzi wa zahanati hiyo kwa kusongeza mchanga na kuchota maji, hatua aliyosema imeonyesha mshikamano na uzalendo wa hali ya juu. Alisema amefurahishwa na ushiriki huo na ndiyo sababu ameungana nao moja kwa moja katika kazi.
Dkt. Biteko alibainisha kuwa lengo la Serikali ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, akieleza kuwa ujenzi wa Zahanati ya Butinzya ulianza mwaka 2018, na Serikali imejipanga kuhakikisha unakamilika ifikapo Juni 2026 ili wananchi, hususan akina mama na watoto, waanze kupata huduma kwa urahisi.
Aliongeza kuwa sambamba na ujenzi wa zahanati, kutajenga pia choo cha wagonjwa ili kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya. Aliwahimiza wananchi kutochoka wala kukata tamaa, bali waendelee kushirikiana na Serikali katika kuharakisha maendeleo ya kijiji chao.
“Mimi natamani kabla ya mwezi wa sita wananchi waanze kupata huduma za afya, hasa huduma za mama na mtoto,”alisema Dkt. Biteko.Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Butinzya, Adelina Mathias, alimshukuru Mbunge kwa kuanza kutekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Alisema kukamilika kwa zahanati hiyo kutapunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutoka Butinzya hadi Ushirombo kufuata huduma za afya, pamoja na changamoto za ndugu kwenda kuwasalimia wagonjwa.
Diwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Chenya, akitoa shukrani zake, pia alisema zahanati ya Sinamila tayari imepokea vifaa mbalimbali vya awali, na kumpongeza Dkt. Biteko kwa mchango wake mkubwa katika kuleta maendeleo. Aliongeza kuwa wananchi wanampenda Mbunge wao, wanamwamini na wamefurahi kumuona akishirikiana nao bega kwa bega katika ujenzi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, aliwapongeza wananchi wa Butinzya kwa ushirikiano mkubwa wanaouonyesha kwa Mbunge wao na Serikali kwa ujumla, akiahidi kuwa halmashauri itaendelea kupeleka miradi ya maendeleo katika kata hiyo kwa manufaa ya wananchi.

Comments
Post a Comment