DE-D AMPONGEZA MBUNGE KWA USHIRIKIANO WAKE NA WANANCHI

Na, Ernest Magashi

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuwa na maono ya kimaendeleo na kwa ushirikiano wake wa karibu na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.Pongezi hizo zilitolewa baada ya Mbunge Dkt. Biteko kuzungumza na wananchi wa Kata ya Butinzya, wakati walipokuwa wakijitolea kwa pamoja kusomba zege, mchanga, mawe na maji katika mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Butinzya. Adelina alisema ushirikiano huo unaonesha uongozi wa mfano unaowahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo yao.Akizungumza na wananchi hao, Dkt. Biteko aliwashukuru kwa kumchagua kwa kura nyingi pamoja na kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.Aidha, aliwahimiza kuendelea kudumisha mshikamano, umoja na moyo wa kujitolea katika miradi ya maendeleo ya vijiji na kata.Dkt. Biteko alisema ameanza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo, ikiwemo ujenzi wa zahanati, ili kufikia malengo ya Serikali ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.Aliongeza kuwa Serikali pia inatarajia kufanya ukarabati wa miundombinu ya madarasa na vyoo katika shule za msingi 23 wilayani Bukombe, ikiwa ni sehemu ya ahadi na juhudi za kuimarisha sekta ya elimu katika jimbo hilo.

Comments