Jeshi la polisi mkoani Geita linamshikilia dalali wa mahakama Wema Haibe (38) kwa tuhuma za kuiba kiasi cha sh22 milioni baada ya kuuza nyumba aliyokuwa amekabidhiwa na mahakama.
Taarifa ambayo imetolewa na Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita, kamishina msaidizi mwandamizi wa jeshi hilo Safia Jongo imeeleza kuwa, mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo wakati akitekeleza dhamana ya amri ya mahakama ya mwanzo ya wilaya ya Geita kituo cha Nyankumbu mjini Geita.
Mahakama hiyo ilikuwa imetoa amri ya kuuza nyumba hiyo iliyopo maeneo ya Fadhiri Bucha kata ya Buhalahala wilayani Geita kufuatia talaka Na.65/2024 ya wanandoa Joseph Kalinda na Ndimira Kasisi.
Mtuhumiwa aliuza nyumba hiyo mnamo Aprili 4,2025 kwa Tatizo Balanzila (56)kwa kiasi cha sh 22milioni na kuweka fedha hiyo kwenye akaunti yake binafsi badala ya akaunti ya mahakama kama alivyokuwa ameagizwa.
Jeshi la polisi mkoani humo limewataka wananchi na madalali wa mahakama kuendelea kutimiza wajibu wao kwa mjibu wa sheria kwani halitasita kuchukua hatua kwa wanaokiuka sheria.

Comments
Post a Comment