MAKARANI ZAIDI YA 600 WAAPISHWA KUSIMAMIA UCHAGUZI MKUU KWA UADILIFU BUKOMBE

Na, Henry Evarist 

Makarani waongoziji 620 wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika Jimbo la Bukombe, mkoani Geita, wameapishwa leo katika hafla maalum iliyofanyika katika eneo la Shule ya Sekondari Bulangwa, Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.Zoezi hilo limeongozwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Bukombe, Zedekiah Solomon Osano, likihudhuriwa na maafisa wasaidizi, pamoja na waandishi wa habari.Makarani hao wametoka katika tarafa za Siloka, Ushirombo na Bukombe zinaunda wilaya ya Bukombe na wameapa kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uadilifu, na kwa mujibu wa sheria, pamoja na kutunza siri za uchaguzi na kujitoa uanachama wa vyama vya siasa, kama inavyotakiwa na sheria za uchaguzi nchini.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Osano aliwataka makarani hao kuzingatia kiapo chao na kuwa mfano wa uwajibikaji, uadilifu na uaminifu katika kipindi chote cha uchaguzi.
“Kumbukeni kwamba msemaji mkuu kuhusu masuala ya uchaguzi ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo au wa Kata pekee. Epukeni kutoa taarifa zisizo rasmi au kuzungumza na vyombo vya habari bila idhini ya Tume,” alisisitiza Osano.

Baada ya kiapo, Msimamizi huyo wa uchaguzi alifungua rasmi mafunzo ya siku moja kwa makarani hao, yaliyolenga kuwaongezea uelewa juu ya taratibu, kanuni na sheria za uendeshaji wa uchaguzi.Mafunzo hayo yanahusisha makarani waongozi wa wapiga kura, wasimamizi wa vituo, na wasaidizi wa wasimamizi wa vituo, ambao watatekeleza majukumu yao katika vituo vya kupigia kura wakati wa uchaguzi mkuu.

Osano alibainisha kuwa Jimbo la Bukombe lina jumla ya vituo 586 vya kupigia kura vinavyopatikana katika kata 17 za wilaya hiyo.“Dhamana mliyopewa ni kubwa na nyeti kwa mustakabali wa taifa. 

Hivyo mnapaswa kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Miongozo na Maelekezo yote ya Tume,” alisema.

Aidha, aliwakumbusha makarani hao kuwa tangu siku ya uteuzi wao, wanachukuliwa kuwa watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa Kifungu cha 20 cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, hivyo wanapaswa kuwajibika moja kwa moja kwa Tume na si kwa mamlaka nyingine yoyote.“Ni marufuku kutoa taarifa au nyaraka za uchaguzi kwa mamlaka au mtu yeyote bila ridhaa ya Tume. 

Simamieni viapo vyenu vya kutunza siri na kujitoa uanachama wa chama cha siasa katika kipindi chote cha uchaguzi,” aliongeza Osano.Mafunzo hayo yamehitimishwa kwa wito kwa makarani wote kufanya kazi kwa ushirikiano, kuhakikisha vifaa vya uchaguzi vinakaguliwa kabla ya matumizi, na kufika vituoni mapema siku ya kupiga kura ili kuhakikisha maandalizi yanakamilika kabla ya muda wa kupiga kura kuanza.

“Tume inategemea nyinyi kuwa mabalozi wa haki, amani na uwazi katika vituo vyenu. Fanyeni kazi kwa weledi ili uchaguzi wa mwaka 2025 uwe huru, wa haki na wenye kuaminika,” alihitimisha Bw. Osano.

Comments