Mgombea udiwani wa Kata ya Ikungwigazi, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Faustine Kapolu, ameahidi kuleta maendeleo na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya kijamii iwapo atachaguliwa.Kapolu alitoa ahadi hiyo wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata hiyo, ambapo alieleza kuwa atazunguka kila kitongoji kuomba kura na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi ili azitatue kwa vitendo.
“Nia yangu ni kuwatumikia wananchi wa Ikungwigazi kwa uaminifu na kuwawakilisha ipasavyo. Nitaweka mkazo kwenye elimu, afya, miundombinu na usimamizi bora wa miradi ya maendeleo,” alisema Kapolu.
Katika mkutano huo, mgombea ubunge wa Jimbo la Mbogwe, Fagason Alon, aliungana na Kapolu na kuwaomba wananchi wawaunge mkono kwa kura zao, akisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya hiyo.
“Naomba wananchi wa Ikungwigazi muendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimedhihirisha uwezo wa kuleta maendeleo. Pamoja na changamoto zilizopo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha dhamira ya kweli kwa maendeleo ya Wilaya ya Mbogwe. Ni mama mwenye upendo na maono,” alisema Fagason.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Evarist Gervas, aliwataka mabalozi wa nyumba 10 pamoja na wenyeviti wa vitongoji na vijiji kuhamasisha wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura kwa ajili ya Rais, Mbunge na Diwani ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika kata hiyo.
“CCM ni chama tofauti na vyama vingine vya siasa. Tunaingia kwenye uchaguzi tukiwa tayari kwa kazi. Tumeshajipanga kwa mujibu wa ilani yetu ya uchaguzi ili kuwaletea maendeleo wananchi wa kila kona ya nchi,” alisema Gervas.
Comments
Post a Comment