Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe, Mkoa wa Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameahidi kuanza na kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Ituga, iliyopo Kata ya Bukombe, mara baada ya uchaguzi mkuu.
Lengo la hatua hiyo ni kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.Dkt. Biteko alitoa ahadi hiyo katika mkutano wake wa kampeni wa 22, akiwaomba wananchi wamchague yeye pamoja na Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na madiwani wa chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura, akisema kuwa hatua hiyo itakuwa ni sehemu ya kuharakisha maendeleo, ikiwemo ukamilishaji wa zahanati hiyo.
“Naombeni wanaituga mchaguwe CCM. Baada ya uchaguzi nitaanza kukamilisha zahanati hii. Tumeshapata mabati, tunatafuta mbao. Wananchi wapate huduma za afya karibu. Kazi yenu ni kupiga kura nyingi, mengine niache mimi,” alisema Dkt. Biteko.
Aidha, alieleza kuwa tayari mtandao wa maji utataongezwa hadi vijiji vya Mkange, Ilalwe na maeneo mengine, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.
Aliongeza kuwa, baada ya uchaguzi, CCM imelenga kuongeza visima na kuibadilisha sura ya Ituga ndani ya miaka 15 ijayo kwa kuboresha miundombinu ya afya na huduma zingine za kijamii.
“Tutajenga zahanati hii kwa kiwango kitakachowezesha ibadilishwe kuwa kituo cha afya, ili wananchi waweze kupata huduma za upasuaji hapa hapa Ituga,” aliongeza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Bukombe kupitia CCM, Rozalia Masokola, alimuomba Dkt. Biteko kuhakikisha zahanati ya Ituga inakamilika mara baada ya uchaguzi, sambamba na kuendeleza miradi mingine ya maendeleo katika kila kijiji cha kata hiyo.

Comments
Post a Comment