DKT. BITEKO AWASHUKURU NA KUWAPONGEZA WALIMU WALIOMFUNDISHA SHULE YA MSINGI , AUPONGEZA UONGOZI WA SERIKALI BUKOMBE

 



Bukombe,- Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri mkuu na waziri wa Nishati ,  amemshukuru  Mwenyezi Mungu kwa kuwakutanisha tena na walimu wake, na kuomba awapumzishe walimu wote waliotangulia mbele za haki. Akizungumza katika tukio linaloendelea la kusherehekea  siku ya maadhimisho ya walimu Bukombe , Dkt. Biteko alisema kuwa ni faraja kubwa kuweza kuonyesha shukrani zake kwa walimu waliomfundisha na kumsaidia katika safari yake ya elimu na taaluma.


Aidha, Dkt. Biteko alimshukuru Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa kufika na kuungana na walimu wa Bukombe. Alisema uwepo wa Waziri Mkuu umewapa walimu moyo na matumaini makubwa kwamba jitihada zao za elimu zinatambuliwa na kuthaminiwa na serikali. “Leo tumepokea mojo kubwa kutoka kwa serikali yetu. Nilijifunza mengi kama msaidizi wa Waziri Mkuu,” alisema Dkt. Biteko, akiongeza kuwa matukio kama haya huimarisha ushirikiano kati ya walimu na viongozi wa serikali.


Dkt. Biteko pia alikumbuka kwa heshima walimu wake wa zamani waliomfundisha, akiwataja Mwalimu Kolesi Sogolo, Thomas Msangi, na Nicholaus Kasendamila, akisema kuwa mchango wao katika maisha yake ya kielimu na kitaaluma hauwezi kupuuzwa. “Kila mmoja wenu amefanya kazi isiyo na kifani katika kuwaandaa vizazi vya kesho,” aliongeza.


Tukio hili limewashirikisha walimu mbalimbali kutoka Bukombe, ambao wameshiriki sherehe ya maadhimisho huku wakipata fursa ya kuungana na viongozi wa ngazi ya juu. Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa kuendeleza elimu bora, akisema kuwa walimu ni msingi wa maendeleo ya taifa na kuhamasisha jamii kuelekea mafanikio ya pamoja.







Comments