Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ametoa wito kwa Watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025, kushiriki katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Akizungumza leo, Oktoba 5, 2025, wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la AICT Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Dkt. Biteko aliwahimiza wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura, akisisitiza kuwa kura ya kila mmoja ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa."Natoa wito kwa wote waliojiandikisha kupiga kura, wajitokeze kwa wingi Oktoba 29. Kura yako ni haki ya kikatiba na ina uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo yako," alisema Dkt. Biteko.
Aidha, alieleza kuwa Serikali imeandaa vituo vingi vya kupigia kura nchi nzima ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi na kuongeza ushiriki wa wapiga kura.Katika ibada hiyo, Dkt. Biteko pia aliwatangazia waumini wa kanisa hilo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya ziara wilayani Bukombe wiki ijayo.
“Naomba mpokee salamu nyingi kutoka kwa Mheshimiwa Rais Samia, ambaye Oktoba 12 atakuwa katika Wilaya yetu ya Bukombe. Nawaomba mjitokeze kwa wingi kumpokea, kwani Mheshimiwa Rais anatupenda sana,” alisisitiza Dkt. Biteko.
Comments
Post a Comment