Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameendelea na ziara zake za kampeni kwa kutembelea kata na vitongoji mbalimbali ndani ya wilaya hiyo, akiwataka wananchi kumpa kura za kishindo ili aweze kutekeleza ilani ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akiwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Butinzya, Dkt. Biteko alieleza vipaumbele vya maendeleo vitakavyotekelezwa endapo atachaguliwa tena, akisisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara."Katika kipindi kilichopita hatukuwa na barabara, lakini leo hii barabara kutoka Butinzya hadi Isemabuna na maeneo mengine zimefunguliwa. Changamoto ya maji tunaifanyia kazi na lengo letu ni kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa umbali usiozidi mita 400. Pia tunajenga zahanati mpya, kuongeza vyumba vya madarasa na kukarabati shule zilizochakaa," alisema Dkt. Biteko.
Amewataka wananchi wa Butinzya kumchagua Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi ili aweze kuendeleza kasi ya maendeleo, akieleza kuwa Rais ana nia ya dhati kuhakikisha kila Mtanzania anaishi maisha bora kupitia utekelezaji wa ilani ya CCM."Acheni kusikiliza maneno yasiyojenga wala kuleta maendeleo. Umoja na mshikamano ndiyo msingi wa ushindi wetu. Wilaya ya Bukombe itajengwa kwa umoja bila kelele za maneno maneno," aliongeza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Tanzania Bara, Mussa Mwakitinya, alieleza kuwa ilani ya CCM imeweka bayana malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kukuza uchumi wa Mtanzania na kuimarisha ustawi wa jamii.Aidha, mgombea udiwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Mathias, aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo na kuwaomba wachague wagombea wote wa CCM. Aliahidi kuwa, iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza, watashughulikia changamoto zote zinazowakabili wananchi wa kata hiyo, hasa suala la upatikanaji wa maji safi na salama.
Comments
Post a Comment