Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, amewashukuru wananchi wa Bukombe kwa heshima kubwa na ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha kampeni kilichofanyika katika kata 17 za wilaya hiyo.
Dkt. Biteko alitoa shukrani hizo Oktoba 27, 2025, wakati wa mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika katika Uwanja wa CCM, kata ya Igulwa.
“Nataka niwaambie wana Bukombe, huwa mnanipa deni kubwa sana moyoni mwangu hamjui tu. Najiona mnanipa stahili nisiyostahili, kwa sababu kama binadamu nina mapungufu yangu mengi, lakini mnaendelea kuniheshimu,” alisema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko aliwashukuru vijana wa hamasa kwa mchango wao mkubwa katika kampeni, na kuwaahidi kuwapa ushirikiano wa karibu katika nyanja zote.
“Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha vijana wa hamasa hawaishii kwenye kampeni pekee. Hawa ni vijana wetu, lazima tuwakomboe. Kila mara tunapowaita mnaitika wito mnanipa deni na heshima kubwa sana,” alisema.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Biteko aliwakumbusha wananchi kuwa siku hii niya kufunga kampeni katika jimbo la Bukombe, na kuwataka kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura kwa wagombea wote wa CCM, ili chama hicho kiendelee kuongoza serikali.
“Leo ni siku ya kukumbushana tu mambo tuliyozungumza katika siku 55 za kampeni. Kazi iliyosalia sasa ni moja kwenda kupiga kura. Naomba watuwema wa Bukombe, siku mbili zilizobaki tuendelee kukumbushana. Baada ya kupiga kura, mengine niachieni mimi,” alisisitiza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholas Kasendamila, alisema kuwa kampeni za ngazi ya mkoa zimehitimishwa rasmi, na sasa chama kinatarajia mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufunga kampeni za kitaifa jijini Mwanza Oktoba 28, 2025 ambae pia ni mwenyekiti wa chama hicho kitaifa.
“Kampeni zinafikia tamati leo kwa ngazi ya mkoa. Oktoba 29, 2025 ni siku muhimu kwa wananchi wote siku ya kupiga kura, haki yao ya kikatiba. Nawasihi mjitokeze kwa wingi kumpigia kura Dkt. Samia kwa urais, Dkt. Biteko kwa ubunge, na madiwani wote wa CCM,” alisema Kasendamila.

Comments
Post a Comment