Na Ernest Magashi
Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameahidi kuongeza idadi ya zahanati na kuleta gari la kubeba wagonjwa katika Kata ya Runzewe Mashariki ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa kina mama wajawazito.
Dkt. Biteko alitoa ahadi hiyo katika mkutano wa 21 wa kampeni sake uliofanyika katika Kijiji cha Bulumbaga, Kata ya Runzewe Mashariki, alipokuwa akiwaomba wananchi kumpigia kura ya ubunge pamoja na kura kwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mgombea udiwani.Akihutubia mamia ya wakazi waliohudhuria mkutano huo, Dkt. Biteko aliwashukuru wanachama wa CCM kwa kumchagua bila kupingwa kuwa mgombea ubunge, na kwa kumchagua Mary Nchiba kuwa mgombea wa udiwani, akisema hatua hiyo itawezesha kusukuma mbele maendeleo ya kata hiyo.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika miaka ya nyuma, Dkt. Biteko alisema kuwa zamani huduma za kijamii, hasa afya, zilikuwa duni katika Kata ya Runzewe Mashariki na wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo katika Kijiji cha Ikuzi.
Hata hivyo, alibainisha kuwa kwa sasa huduma zimesogezwa karibu na kwamba zitaimarishwa zaidi baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
“Ndugu wananchi wa Bulumbaga, napenda kuanza kwa kuwashukuru kwa kuja kwa wingi kutuunga mkono wakati tunasimamia miradi ya maendeleo. Asanteni sana. Tuendelee kushirikiana na kupeana moyo. Kazi kubwa yenu ni kupiga kura nyingi kwa Rais Dkt. Samia, mengine niachieni. Maendeleo makubwa yanakuja tutaongeza zahanati na kuleta gari la kubeba wagonjwa,” alisema Dkt. Biteko.Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Runzewe Mashariki, Mary Nchiba, alianza kwa kumpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi kubwa alizofanya kuwaletea maendeleo wananchi wa kata hiyo.
Nchiba aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo wa kampeni na kuwaomba kura kwa ajili ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Biteko kwa nafasi ya ubunge, na yeye mwenyewe kwa nafasi ya udiwani ili aweze kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hakika, Bukombe inasonga mbele kwa juhudi zako tunazozishuhudia kwa macho yetu wenyewe. Inaitendea haki kauli ya "Kusema na Kutenda". Mungu wa mbinguni aendelee kukupa afya njema, nguvu, amani, uwezo na hekima zaidi ya kuwatumiakia want Bukombe na Tanzania yetu. Mkono wa Bwana wetu Yesu Krsito uwe nawe wakati wote wa kampeni na hata siku ya uchaguzi. Big up Biteko.
ReplyDelete