ZAHANATI YA BUFANKA KUPANDISHWA HADHI KUWA KITUO CHA AFYA

Na, Ernest Magashi

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameahidi kuwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, Zahanati ya Bufanka itapandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya ili kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza leo Septemba 20, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Bugelega, Dkt. Biteko alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi, na kupunguza changamoto za upatikanaji wa matibabu hasa kwa kinamama wajawazito na watoto.Mbali na ahadi hiyo, Dkt. Biteko pia aliahidi ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari) pamoja na kuandaa gari la wagonjwa (ambulance) litakalosaidia usafiri wa haraka kwa wagonjwa wa rufaa wanaopelekwa Hospitali ya Wilaya.

"Bugelega haina shida ya kuleta maji, bali tunahitaji kusambaza maji yaliyopo ili kila eneo lifikiwe. Vijiji sita vina umeme tayari, sasa tunapeleka kwenye vitongoji tisa vilivyobaki. Pia tutahamasisha wanawake kuachana na matumizi ya mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ya majiko ya umeme," alisema Dkt. Biteko.

Aliongeza kuwa shule za msingi ambazo bado hazijasajiliwa zitasajiliwa rasmi, na zile zenye miundombinu chakavu zitakarabatiwa. “Awali tulianza na maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi. Sasa tutaelekeza nguvu kwenye ukarabati na uboreshaji wa shule zilizopo,” alisema.Dkt. Biteko aliwahimiza wananchi wa Bugelega kumpigia kura yeye pamoja na wagombea wenzake wa CCM, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana pasipo ushiriki wa wananchi kwenye uchaguzi.

“Najua wananchi hawahitaji maneno, wanahitaji maendeleo. Miaka mitano ijayo tutashuhudia maendeleo makubwa zaidi kuliko iliyopita. Nipeni kura zenu pamoja na Leonard Lubigisa, naahidi ushirikiano mkubwa zaidi,” alisisitiza Dkt. Biteko.

Aidha, aliwahimiza wananchi kumpigia kura mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili ashinde kwa kishindo, akisema kuwa chini ya uongozi wake, serikali imeonyesha dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo wananchi wa maeneo ya vijijini hasa jimbo la Bukombe. Awali Mgombea Udiwani wa Kata ya Bugelega, Leonard Lubigisa, alitumia nafasi hiyo kumshukuru Dkt. Biteko kwa jitihada zake za kuondoa kero ya muda mrefu ya daraja la Bugelega Mbogwe ambalo sasa linapitika wakati wote, hata wakati wa mvua.

Lubigisa pia aliomba Zahanati ya Bufanka ipandishwe hadhi kuwa Kituo cha Afya, pamoja na ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti na wodi ya mama na mtoto ili kuboresha huduma kwa wakina mama wajawazito na watoto wachanga.

Naye Mgombea Udiwani wa Viti Maalum, Pili Kondela, aliwataka wananchi wa Bugelega kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025, na kuwachagua wagombea wa CCM ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika kata hiyo na taifa kwa ujumla.


 

Comments