WAZIRI MKUU ALIPONGEZA SHIRIKA LA STAMICO KUSAIDIA WACHIMBAJI MITAMBO YA KISASA


Na, Salum Maige

Waziri mkuu Kasim Majaliwa amelipongeza shirika la madini la Taifa STAMICO kutekelezwa matakwa ya Serikali ya kusaidia kutoa mitambo ya kisasa kwa wachimbaji wadogo wa madini ili kuondokana na matumizi ya zana duni.

Waziri mkuu ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea banda la shirika hilo kwenye maonyesho ya 8 ya Kitaifa ya Teknolojia ya madini yanayofanyika mjini Geita alipowasili katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua maonyesho hayo.Amesema, serikali itaendelea kushirikiana na wachimbaji wadogo kwa kuwawezesha vifaa mbalimbali vya kisasa ikiwa ni mpango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwasaidia wachimbaji ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Akiwa katika banda hilo amejionea shughuli zinazofanywa na chama cha wachimbaji wanawake Tanzania(TAWOMA) vijana wachimbaji na watu wenye changamoto ya kusikia waliowezeshwa na shirika hilo ambao moja ya shughuli wanazofanya ni kuchimba madini na uunganishaji wa madini kabla ya kuyauza.“Hongereni sana STAMICO mnafanya kazi nzuri nimeshuhudia mitambo ya kisasa kabisa ambayo mingine wamebuni wachimbaji wenyewe ,hii ni hatua kubwa sana, wachimbaji niwatoe wasiwasi, serikali itaendelea kuwasaidia kupitia shirika hili” alisema Majaliwa.

Awali akitoa taarifa ya shirika hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Deusdedith Magala alionyesha shughuli zinazofanywa na shirika hilo kuwa ni pamoja na kutoa mitambo ya kisasa kwa wachimbaji, ukiwemo mtambo wenye uwezo wa kuchoronga mita 3,000 kwenda chini.

“Mheshimiwa waziri mkuu mtambo huu ni mtambo mkubwa zaidi barani Afrika na ni teknolojia ya kisasa kabisa. Tumewezesha wachimbaji wadogo na wakubwa ili waweze kuchimba kirahisi kwa kutumia mitambo ya kisasa” amesema Magala.Aidha, Magala amesema, shirika hilo kwa kushirikiana na vijana limeweza kuibua vijana waliobuni mtambo wa kutoa mawe chini ya ardhi kilo 150 hadi 200 zaidi ya mita 100 huku uwezo wake ni kuvuta tani 20 kwa siku.“Mtambo huu mheshimiwa waziri mkuu unatokana na injini ya pikipiki aina ya guta umesaidia wachimbaji ambao hapo awali walikuwa wakivuta tani 2 hadi 3 za mawe kutoka chini kwa siku lakini kwa kutumia mtambo huo wanavuta tani 20 kwa siku,  hivyo umeleta mageuzi na mabadiliko makubwa katika sekta ya madini” alisema mmoja wa vijana hao.

Magala amewataka wananchi kutembela banda hilo kupata elimu ya uchimbaji katika kipindi hiki cha maonyesho yaliyoanza septemba 18 na yanataraiwa kuhitimishwa septemba 28,mwaka huu Tumewezesha. 

Comments