WAJA AWAKOSHA WANANCHI AKIJINADI UZINDUZI WA KAMPENI


Na, Salum Maige

Mamia ya wananchi wamejitokeza wakati Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Geita kikizindua kampeni zake za uchaguzi mkuu katika jimbo la Geita mjini na kikiwanadi wagombea wake kwa wananchi wa nafasi ya ubunge Mhandisi Chacha Wambura na wanaowania nafasi ya udiwani kata 13.

Kampeni hizo zimezinduliwa katika kijiji cha Nyaseke kata ya Bulela na Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Geita Barnabas Mapande ambaye alikuwa mgeni rasmi na kudai kuwa zipo sababu za kuwaamini wagombea hao kutokana utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta zote.Mapande amesema, katika mkoa wa Geita kwa upande wa elimu kabla ya Serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani shule za sekondari zilikuwa 60 lakini zimeongezeka hadi shule 108 na kwa shule za msingi, shule zilikuwa 208 na zimeongezeka hadi 314.

“Hivyo niwaambie wananchi kichagueni chama cha mapinduzi ambacho, tunaposema mkichague chama hiki, tunamanisha kwa sababu wagomnbea wake wako makini na wana uwezo wa kuwatumikia wananchi na sisi kama chama tutawasimamia,” Amesema Mapande.Mapande amemkabidhi Ilani Mgombea ubunge na kumtaka kwenda kuhakikisha anasimamia utekelezaji wake.Kwa upande wake mgombea ubunge jimbo la Geita mjini Mhandisi Chacha Wambura alimaarufu Waja ametaja vipaumbele vyake vitano ikiwemo elimu, afya, barabara, maji na ajira kupitia sekta ya madini.Kabla ya kufafanua vipaumbele hivyo aliwaahidi wananchi wa kata ya Bulela kuwa, atahakikisha wananchi wanafikiwa na huduma za maji, kusimamia ujenzi wa barabara inayounganisha wananchi wa Bulela, Shiloleni na wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

Pia, ameahidi wananchi hao kuwa, atasimamia masuala ya afya kwa kuboresha miundombinu na kutoa gari la wagonjwa sambamba na majosho ya kuogesha mifugo yanafufuliwa pamoja na mabwawa ya kunyweshea mifugo na wakulima wanafikiwa na mbolea za ruzuku kwa wakati.“Niwaambie tunaenda kufuta tatizo la uhaba wa walimu, uhaba wa vyumba vya madarasa, uhaba wa madawati ,kwani bila elimu hatuwezi kupata maendeleo ,lazima changamoto hizi tukaziondoe” amesema Wambura.

Awali Katibu wa Itikadi, uenezi na Mafunzo wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Geita Gabriel Nyasiru amewataka wagombea wa CCM kwenda kusimamia makusanyo ya halmashauri ili wananchi waweze kunufaika na uongozi wao.

“Hata sisi chama cha mapinduzi tunaenda kuwasimamia kuhakikisha wanawajibika kwa wananchi kwa kusimamia mapato ya Serikali kwenye halmnashauri,”amesema Nyasiru.


 

Comments