Mgombea Udiwani wa Kata ya Masumbwe, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita Kupitia chama cha mapinduzi (CCM), Peter Mnunke, amewaomba wananchi kumpa ushirikiano ili aweze kuwaletea maendeleo ya kweli katika kata hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika katika Kijiji cha Ilangale, Mnunke aliahidi kusukuma mbele agenda ya maendeleo kwa kusogeza huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo maji safi, miundombinu ya barabara, umeme katika kila kitongoji, pamoja na kuboresha shule za msingi na sekondari.
Amesema, iwapo atachaguliwa, atahakikisha shule zitakazofanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba na kidato cha nne zinapewa motisha ili kuinua kiwango cha elimu katika kata hiyo.
“Nitaenzi na kuheshimu mawazo ya kila mmoja. Nitasikiliza, kutathmini na kuyafanyia kazi kwa kuzingatia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Viongozi kuanzia ngazi ya chini nitawaheshimu, kwa kuwa maendeleo ni matokeo ya ushirikiano,” alisema Mnunke.
Aidha, alitumia jukwaa hilo kuwaomba wananchi kumpigia kura Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa atashirikiana nae pamoja na Mgombea Ubunge katika kusukuma mbele miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita, Aman Nswila, aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanawachagua kwa kura nyingi wagombea wa CCM katika nafasi zote ili kutekeleza dhamira ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi.
Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Patrick Msafi, alimuelezea Mnunke kama kijana mchapa kazi, aliyewahi kulitumikia Serikali ya Kijiji kwa mafanikio, na kuwaomba wananchi wamchague ili aweze kuleta mabadiliko chanya katika Kata ya Masumbwe.

Comments
Post a Comment