Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Kasim Majaliwa amepongeza taasisi ya benki ya AZANIA iliyopiga hatua kubwa ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kutumia zana duni.
Majaliwa ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea banda la AZANIA katika maonyesho ya 8 ya kitaifa ya teknolojia ya madini kabla ya kufungua maonyesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan Bombambili manispaa ya Geita.
Amesema, mkakati wa benki hiyo ni wa kuigwa na kwamba nia yake ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali za kuwakwamua wachimbaji wadogo ili wachimbe kwa teknolojia ya kisasa.
Akitoa taarifa ya benki hiyo mbele ya waziri mkuu, meneja wa benki ya AZANIA tawi la Geita Roda Baluya amesema, benki hiyo imekuwa bega kwa bega na wachimbaji wadogo na wakati.
Amefafanua kuwa, benki hiyo imekuwa ikiwawezesha wachimbaji kutumia teknolojia sahihi kwa kuwapa fedha kununua mitambo mbalimbali ikiwemo ya kuchakata madini(CIP) ikiwa ni mpango wa benki hiyo kuwatoa wachimbaji kwenye matumizi ya zana duni.
“Mheshimiwa waziri mkuu kuongezeka kwa CIP hapa Geita inatokana na huduma tunazozitoa benki ya AZANIA kwa wachimbaji wadogo kwa kuwawezesha fedha” alisema Roda. Kadhalika, amesema benki hiyo imekuwa ikiwasaidia wachimbaji kuwapa elimu ya kutumia huduma za fedha kwa njia ya kidijitali kwani wachimbaji wengi wamekuwa wakitembea na fedha mikononi jambo ambalo ni risiki kwao.
Meneja huyo amewasisitiza wachimbaji kufika katika banda la benki ya AZANIA kupata elimu ya huduma zinazotolewa na benki hiyo ikiwepo mikopo kwa wachimbaji wadogo, wachuuzi wa mboga mboga, wajasiriliamali, machinga na akina mama ntilie.
Maonyesho hayo yaliyoanza septemba 18 yanatarajiwa kuhitimishwa septemba 28,mwaka huu.

Comments
Post a Comment