Na, Ernest Magashi
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameahidi kwamba baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, Kituo cha Afya Lyambamgongo kitaanza rasmi kutoa huduma za upasuaji.
Dkt. Biteko alitoa ahadi hiyo leo, Septemba 19, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Lyambamgongo, alipokuwa akiwaomba wananchi kumpigia kura yeye pamoja na Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mbali na huduma za upasuaji, Dkt. Biteko ameahidi kuleta gari la kubeba wagonjwa (Ambulence) ili kuwasaidia wananchi wanaopewa rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya wasisubiri kwa muda mrefu kusafirishwa.
Alisema maendeleo yaliyopatikana katika miaka iliyopita yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na viongozi wao. Akitolea mfano, alisema"Barabara ya Ifunde kwenda Kagwe ilikuwa haipitiki, lakini leo tumefungua na inapitika vizuri.
"Najua wananchi wa Lyambamgongo hawahitaji maneno, wanahitaji maendeleo. Na miaka mitano ijayo itakuwa ya maendeleo makubwa zaidi kuliko iliyopita," Alisema Dkt. Biteko.
Alibainisha pia kuwa Kata ya Lyambamgongo ina vitongoji 14, kati ya hivyo saba vina umeme na saba havina, aliahidi kuwa baada ya uchaguzi vitongoji vyote vitapata umeme.
"Nipeni Shitobelo, nitampa ushirikiano mkubwa zaidi ya miaka mitano iliyopita. Hana majungu, anafuatilia maendeleo. Kwa hiyo, tupeni kura wagombea wote wa CCM,"alisema Dkt Biteko.
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata ya Lyambamgongo, Boniphace Shitobelo, alisema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Dkt. Biteko, imeleta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali, uboreshaji wa barabara, Vifaa vya maabara na maji safi.

Comments
Post a Comment