Salum Maige
Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Geita imewaonya wanachama wake kuendekeza makundi yanayotokana na kura za maoni badala ya kushikama kuhakikisha wagombea wateule kupitia chama hicho wanashinda kwenye uchaguzi mkuu wa oktoba 29,mwaka huu.
Onyo hilo limetolewa na mwenyekiti wa Jumuiya hiyo wilaya ya Geita Robert Nyamaigolo alikutana na viongozi jumuiya hiyo ngazi ya kata ikiwa ni hatua ya kuvunja makundi na kuwaunga mkono wagombea waliopitisha na vikao halali vya ngazi ya maamzi ndani ya chama hicho.
“Twendeni tukazungumze lugha moja katika kipindi hiki, kila nafasi ilikuwa moja ,hata wangejitokeza wagombea 80, kati yao angaepatikana mmoja ,anapopatikana huyo mmoja lazima tushikamane kuhakikisha tunamuunga mkono ili ashinde” amesema Nyamaigolo.
Amesema chama Jumuiya haitasita kuwachukulia hatua wanachama wake watakaobainika wanaendekeza makundi ambayo hayana mantiki katika uchaguzi huu.
“Nendeni mkavunje makundi yenu, na kila mmoja mlioko hapa mkapeane majukumu ya kuhakikisha chama cha mapinduzi CCM kinashinda ,nendeni mkaweke vikao ,muweke mipango ya namna gani wagombea wetu wanashinda, lakini kama kuna mwanachama anaendekeza makundi kwenye jumuiya yangu sitosita kumchukulia hatua” , amesema mwenyekiti huyo.
Awali akimkaribisha mwennyekiti huyo kuzungumza kwenye kikao hicho, Katibu wa Jumuiya hiyo wilaya ya Geita Ramadhan Ndago amesema lengo la kukutana ni kujadili njia nzuri itakayoleta mafanikio ya wagombea wa CCM kushinda ngazo zote Diwani, ubunge na Rais.
“Kikao hiki ni cha dharula, ni kikao muhimu sana kwenye kipindi hiki cha uchaguzi, muda wowote tunaweza kuwaita, hivyo tuvumiliane lengo ni kuhakikisha tunashikamana tunaenda pamoja kukipambania chama chetu(CCM) kinashinda nafasi zote” amesema Ndago.

Comments
Post a Comment