Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, amewaahidi wananchi wa jimbo hilo maendeleo ya pamoja ikiwa ni pamoja na ukarabati wa shule za msingi na kukamilisha ujenzi wa zahanati mara baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Dkt. Biteko alitoa ahadi hizo Septemba 30, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Igulwa, ambapo aliomba kura kwa ajili yake, mgombea urais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea udiwani wa kata hiyo, akisema kuwa kura hizo ni msingi wa kudai maendeleo.
Alisema kuwa anafahamu changamoto zilizopo katika kata hiyo, na kwamba moja ya mikakati yake ni kuhakikisha taa za soko la zamani marufu (kariaako) zinawekwa ili kurahisisha shughuli za kiuchumi, hasa kwa wafanyabiashara wanaofanya kazi hadi usiku. Alisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza kipato cha wananchi.
"Niwambie watu wema wa Bukombe, mama yetu Rais Dkt. Samia anatupenda sana. Tulikuwa na stendi ambayo mvua ikinyesha tunapita kwenye maji mengi kama majarubio. Mama Samia akasema tupige chini, tujenge stendi mpya inayoendana na hadhi ya Ushirombo. Akasema pia tupige chini soko la zamani sasa ujenzi wa soko jipya unaendelea," alisema Dkt. Biteko.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na juhudi kubwa za kuleta maendeleo katika mji wa Ushirombo makaomakuu ya wilaya ya Bukombe kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na uwekaji wa taa za barabarani, ujenzi wa barabara za lami, na uboreshaji wa huduma za kijamii.
"Barabara ya kutoka Ushirombo kwenda Katoro sasa inajengwa kwa kiwango cha lami. Hili ni suluhisho la changamoto ya muda mrefu," alieleza.Kuhusu rasilimali za madini zilizopo katika wilaya hiyo, Dkt. Biteko alisema kuwa awali maeneo mengi ya madini yalikuwa ndani ya Pori la Kigos ambako wananchi walikuwa wakinyanyaswa na kuteseka wakitafuta riziki yao.
"Pori lile lilikuwa limegeuka laana kwa watu wa Bukombe. Nilimfuata mama Rais na kumweleza kuhusu mateso ya wananchi. Alikubali, na sasa watu wanafanya kazi kwa bidii, wanachimba dhahabu bila bughudha. Hakuna majungu tena, sasa wanajishughulisha kukuza uchumi," alisema Dkt. Biteko kwa msisitizo.
Awali, mgombea udiwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga, aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa kampeni. Aliahidi kuendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo itakayoletwa na Dkt. Biteko iwapo atachaguliwa kuwa diwani.
"Miradi yote iliyopo Igulwa imeletwa na Dkt. Biteko. Tumuunge mkono ili azidi kutuletea maendeleo zaidi," alisema Mabenga.

Comments
Post a Comment