Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwekeza katika elimu ya watoto wao ili kuwawezesha kuingia katika soko la ajira na kujiajiri.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Musangila, Kata ya Runzewe Magharibi Septemba 16,2025 Dkt. Biteko alisema kuwa licha ya mafanikio mengi ya maendeleo yaliyopatikana, bado elimu ni msingi wa maendeleo ya kudumu.
“Tumefanya maendeleo mengi, lakini baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, tunahitaji wananchi kupiga kura nyingi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Atatuletea shule za msingi na sekondari, hivyo wazazi somesheni watoto ili waje kulitumikia taifa huwezi kuwa kiongozi bora bila Elimu,” alisema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko pia aliwahimiza wananchi kumpigia kura pamoja na madiwani wa CCM ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa kwa kasi zaidi. Alisema Serikali ya CCM imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, umeme kila kijijini, maji safi, na ujenzi wa shule.
“Tumeweka umeme kila kijiji, tumejenga daraja la kuunganisha kijiji cha Lulamba na Msasa, tumeleta maji. Miaka mitano ijayo tunataka maendeleo zaidi, siyo maneno,” alisisitiza Dkt Biteko.
Katika mkutano huo, aliwahimiza wagombea udiwani kuendelea kusaka kura kwa bidii huku akisisitiza mshikamano kati ya viongozi na wananchi baada ya uchaguzi.
Mgombea udiwani wa Kata ya Runzewe Magharibi, Patrick Songolo, alimpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi zake katika kutatua changamoto za wananchi, hususani ujenzi wa shule, usambazaji wa umeme, maji safi, na daraja lililokuwa kero kubwa wakati wa masika.
Naye mkazi wa kiniji cha Musangila, Halma Juma, alisema kuwa anaunga mkono sera za wagombea hao kwa kuwa wamekuwa wakitekeleza ahadi zao kwa vitendo.
“Oktoba 29, nitapiga kura kwa wagombea wanaotekeleza ahadi. Tumeona maendeleo, si maneno tu,” alisema.

Comments
Post a Comment