Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, amewaahidi wananchi wa Kata ya Bulangwa maendeleo makubwa yatakayotekelezwa kwa ushirikiano na madiwani wa CCM baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Bulangwa, Dkt. Biteko alisema ana imani kubwa na kazi zinazofanywa na mgombea udiwani wa kata hiyo, Yusuph Mohammed, akimwelezea kuwa ni kiongozi anayejituma na kushughulikia changamoto za wananchi.“Nimeridhika sana na kazi ya Yusuph.
Anajitoa kwa dhati kutatua changamoto za wananchi. Nawaahidi kuwa kila alichokiomba Yusuph kitatekelezwa baada ya uchaguzi,” alisema Dkt. Biteko.
Aliwahimiza wananchi wa Bulangwa na Bukombe kwa ujumla kuwa wavumilivu, kwani mambo mazuri yanakuja baada ya uchaguzi. Dkt. Biteko alieleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana na mipango zaidi inayokuja.
“Bulangwa tuna zahanati, tuna kituo cha afya, na sasa tutajenga shule mpya ya msingi katika Kitongoji cha Muungano. Pia barabara ya lami kutoka Ushirombo hadi Katoro inaendelea kujengwa, umeme utafikishwa kila kitongoji, na shule zitaongezwa,” alieleza.
Dkt. Biteko aliwaomba wananchi wa Bukombe kumpigia kura kwa wingi yeye pamoja na Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgombea udiwani wa CCM kata hiyo, ili kazi nzuri iendelee kufanyika.
“Nifanyieni hisani kwa kunichagua mimi kwa kura nyingi, mpeni kura nyingi Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Yusuph kwa udiwani. Yote aliyoyaomba yatafanyika, yakiwemo maji safi, kwa kuwa Rais Dkt. Samia amedhamiria kwa dhati kuibadilisha Bukombe,” alisisitiza Dkt. Biteko.
Awali Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Bulangwa, Yusuph Mohammed, alitumia nafasi hiyo kumshukuru Dkt. Biteko kwa juhudi zake, hasa kufanikisha kupatikana kwa sh 350milioni kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Kilimahewa.
“Tunatarajia pia kujenga Shule mpya ya Msingi ya Muungano, kuboresha barabara na kusogeza umeme katika vitongoji vya Kilimahewa na Muungano,” alisema Yusuph.

Comments
Post a Comment