DKT. BITEKO AHAIDI KUJENGA MABWENI SEKONDARI YA BUSINDA


Na Irene Makopudo

Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameahidi kujenga mabweni katika Shule ya Sekondari ya Businda ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, siyo bora elimu.Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Ushirombo, Kitongoji cha Shikalibuga, Dkt. Biteko alieleza vipaumbele vyake vya maendeleo kwa jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya elimu na kuongeza fursa za ajira kwa vijana."Mipango ya wilaya yetu ndiyo kwanza inaanza. Tunaendelea na ujenzi wa chuo cha VETA hapa Ushirombo ili watoto wetu wapate ujuzi wa kujitegemea. Pia, Chuo Kikuu kinatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi mwezi Novemba, hatua ambayo itachochea maendeleo kubaki hapa kwetu," alisema Dkt. Biteko.Aidha, aliwataka wananchi kutochukulia uchaguzi kama chanzo cha migawanyiko, bali kuwa chonzo cha kuleta maendeleo. "Watu wanahitaji maendeleo, siyo maneno matupu. Uchaguzi usitugawanye, maendeleo hayatapimwa kwa maneno bali kwa matokeo ya kazi tunayofanya. Tushikamane kwa ajili ya ustawi wa jimbo letu," alisisitiza.Dkt. Biteko pia aliwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, akisema, "Maendeleo hayawezi kuja kama watu hawatashiriki kupiga kura. Ni lazima tutumie haki yetu ya kidemokrasia ili kuleta mabadiliko chanya.

"Miongoni mwa ahadi alizotoa ni pamoja na Ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari ili wanafunzi wa kike na wa kiume wasome kwa utulivu,Upatikanaji wa bima ya afya kwa wananchi wote,Ufunguzi wa barabara za mitaa ili kurahisisha usafiri, Mikopo kwa vijana kwa ajili ya biashara na ujasiriamali, Uboreshaji wa huduma za maji safi na salama, Kuunganishia umeme wananchi wote pamoja na upatikanaji wa majiko ya umeme kwa matumizi ya nyumbani.

Kwa ujumla, Dkt. Biteko alisisitiza dhamira yake ya kuendeleza maendeleo ya Bukombe kwa kushirikiana na wananchi, na akahimiza mshikamano na ushirikiano wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi. Awali Mgombea Udiwani kata ya Ushirombo Lameck Waragi alimpongeza mbunge kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akifanya ya kuleta maendeleo na kwamba anauhakika Dkt. Biteko kunashule shikizi baada ya uchaguzi zitapata usajili.


 

Comments