DKT. BITEKO AAHIDI MAENDELEO MAKUBWA KWA KATA ZA MJINI


Na, Ernest Magashi

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameahidi kuleta miradi mikubwa zaidi ya maendeleo baada ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 27, 2025 katika Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Dkt. Biteko alisema kata za Katente, Igulwa na nyinginezo za mijini zilikuwa na maendeleo duni mwaka 2015, lakini hali hiyo imebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada za Serikali ya CCM.“Wilaya ya Bukombe ilikuwa na shule moja tu ya sekondari ya kidato cha tano na sita, hospitali moja, na zahanati nne. Umeme ulikuwepo katika vijiji saba pekee. Leo hii tuna vituo vya afya, zahanati nyingi, na umeme umefika karibu kila kijiji; vilivyosalia ni vitongoji vichache tu, ambavyo navyo vitafikiwa baada ya uchaguzi," alisema Dkt. Biteko.Alibainisha kuwa Serikali ya CCM imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, jengo la Halmashauri, soko jipya la kisasa na stendi ya abiria.“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ushirombo hadi Katoro kwa kiwango cha lami, ambayo ujenzi wake unaendelea. Pia, ameruhusu wananchi kuchimba dhahabu katika Pori la Kigosi,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Dkt. Biteko, serikali pia imeanza ujenzi wa miundombinu ya elimu kama vile Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na Chuo Kikuu, ambavyo vitasaidia kuchochea uchumi kwa kuongeza mzunguko wa fedha katika eneo hilo.“Watu hawataki maneno, wanataka maendeleo. Rais Samia amedhamiria kuibadilisha Bukombe,” alisisitiza.Aliwataka wananchi wa Kata ya Katente waliojiandikisha kupiga kura ifikapo Oktoba 29, 2025, kumchagua Rais Samia kwa nafasi ya urais, yeye (Dkt. Biteko) kwa ubunge, na mgombea wa CCM kwa udiwani ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika Wilaya ya Bukombe.

Kwa upande wake, Mgombea wa Udiwani wa Kata ya Katente Tabu Ng’hwani, aliomba kura kwa kueleza mafanikio yaliyopatikana chini ya CCM, yakiwemo ujenzi wa madarasa katika shule za msingi za Igulwa, Bomani, Umoja, Bwenda na Katente.Ng’hwani alitumia fursa hiyo kumpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi zake, na kufichua kuwa kata hiyo imepokea fedha kupitia halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa, stendi ya mabasi na uwanja wa mpira.

Comments