Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameahidi kuendelea kusukuma mbele maendeleo ya miradi ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara katika kata ya Uyovu.
Ahadi hizo amezitoa leo, Septemba 17, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata hiyo, ambapo aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika kwa kupiga kura Oktoba 29, 2025.
kihimiza wananchi kumpigia kura yeye pamoja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Biteko alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kumekuwa na mafanikio makubwa, lakini mengi zaidi yanakuja endapo watapewa ridhaa tena ya kuongoza.
"Nilipoingia bungeni kulikuwa na zahanati tatu tu, leo tunazo zahanati 11. Shule za sekondari zilikuwa sita tu, lakini sasa tunayo moja yenye kidato cha tano na sita. Barabara nazo tunajenga kwa kiwango cha lami, hata hii ya Uyovu kwenda Bugenge itajegwa kwa lami. Tutaongeza zahanati na vituo vya afya. Naomba kura zenu nyingi ili niendelee kudai maendeleo kwa ajili yenu," alisema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko alisema kata ya Uyovu inapaswa kuwa mji wa kibiashara, na serikali ya CCM itahakikisha inavutia wawekezaji kwa kuboresha mazingira ya biashara.
"Tukipewa nafasi tena, tutajenga stendi ya kisasa na kuifanya Uyovu kuwa kivutio cha biashara. Chanzo cha maji safi kipo, lakini kutokana na ongezeko la watu, nitahakikisha tunajenga chanzo kipya cha maji pamoja na kuboresha huduma nyingine muhimu," aliongeza.
Alisisitiza kuwa miaka mitano ijayo kata ya Uyovu itapendeza zaidi, huku akisisitiza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana upendo mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo, hivyo wanapaswa kumchagua kwa kura nyigi.
Kupitia mkutano huo, mgombea udiwani wa kata ya Uyovu, Matayo Kagoma, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kazi kubwa ya maendeleo aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake kuanzia 2020 hadi 2025.
"CCM imeleta vifaa vya vinye sifa ya kugombea na kuleta maendeleo mbalimbali. Zamani tulikuwa na changamoto ya msongamano wa wanafunzi, hasa katika Shule ya Msingi Ibamba, lakini baada ya Dkt. Biteko kuchaguliwa, alitatua changamoto hiyo kwa kujenga madarasa na kuongeza shule za sekondari," alisema Kagoma.
Aliongeza kuwa bado kuna mahitaji ya ujenzi wa shule mpya, vituo vya afya, na zahanati, hivyo wanamhitaji Dkt. Biteko ili kukamilisha miradi hiyo kwa mafanikio zaidi.

Comments
Post a Comment