DKT. BITEKO AAHIDI KUANZA NA UKAMILISHAJI WA ZAHANATI YA ILYAMCHELE


Na Ernest Magashi

Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, ameahidi kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ataanza mara moja kazi ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Ilyamchele, ili kuwaondolea wananchi kero ya kutembea umbali wa kilomita 12 kufuata huduma za afya katika maeneo ya mbali kama Namonge.Dkt. Biteko alitoa ahadi hiyo Septemba 18, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Ilyamchele, kata ya Namonge."Nikuombe Afisa Mtendaji wa kijiji, acha kufanya vikao vingi vinavyochelewesha maendeleo. Fedha za mradi zinapofika zifanye kazi iliyokusudiwa. Wananchi hawahitaji maneno mengi, wanahitaji maendeleo. Natamani Zahanati hii ikamilike ili akina mama wajawazito na wananchi wengine wasitembee umbali mrefu kutafuta huduma za afya," alisema Dkt. Biteko.Aliongeza kuwa ujenzi wa zahanati hiyo umechukua muda mrefu pasipo sababu ya msingi, licha ya kuwepo kwa fedha za ukamilishaji. Aliwaomba wananchi wamchague yeye pamoja na Dkt. Samia, Diwani wa CCM ili ahakikishe kuwa zahanati hiyo inakamilika ndani ya miezi mitatu baada ya uchaguzi.

Pamoja na ukamilishaji wa zahanati hiyo, Dkt. Biteko aliahidi pia kuhakikisha Kituo cha Afya cha Namonge kinapatiwa gari la kubeba wagonjwa (ambulance) ambalo litatumika kuhudumia zahanati zote ndani ya kata ya Namonge. Kwa sasa, wananchi wanalazimika kutegemea gari la wagonjwa kutoka kata ya Uyovu.Akiomba kura za mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Biteko alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imeleta miradi mingi ya maendeleo katika jimbo la Bukombe kwa kata zote, ikiwemo maboresho ya barabara na ujenzi wa daraja la Mhama.

"Rais Dkt. Samia ametuletea fedha nyingi za miradi ya maendeleo. Sasa barabara zimeboreshwa, daraja la Mhama limejengwa, na leo hii mabasi yanafika hadi hapa Ilyamchele na kurudi. Naomba kura nyingi kwa Rais Dkt. Samia Oktoba 29, 2025, ili tuendelee kupata maendeleo zaidi," alisisitiza Dkt. Biteko.Awali, mgombea udiwani wa kata ya Namonge, Mlalu Bundala, alimpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi kubwa alizofanya kuwaletea wananchi maendeleo waliyokuwa wakiyasubiri kwa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme.

"Naomba wananchi waendelee kutuamini ili tuendelee kuwaongoza. Hakika, mambo mazuri yanakuja. Oktoba 29, 2025, pigeni kura nyingi kwangu, kwa Dkt. Biteko na kwa Rais Dkt. Samia  tutapata maendeleo zaidi," alisema Bundala.

Mkazi wa kijiji cha Ilyamchele, John Paschal, alisema sera za wagombea hao ni nzuri na alimpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi zake katika kusukuma mbele ujenzi wa zahanati hiyo.

"Mpaka sasa zahanati imefikia hatua hii kwa nguvu ya mbunge wetu. Tuna imani kuwa baada ya uchaguzi, itakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi," alisema Paschal.


 

Comments