Benki kuu ya Tanzania(BOT) imesema itaendelea kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wakubwa na wadogo kwa bei iliyopo katika ushindani wa soko la dunia ili kutoa faida kwa wachimbaji hapa nchini.
Afisa wa benki hiyo kutoka idara ya masoko ya fedha BOT Rehema Kassim amesema hayo mbela ya Waziri mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea banda la benki hiyo kwenye maonyesho ya 8 ya kitaifa ya teknolojia ya madini mkoani Geita.
Rehema alimweleza waziri mkuu kuwa, benki hiyo kuanzia oktoba 2024 iliweka mkakati wa kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo ikiwa ni hatua ya serikalin kuwa na akiba ya dhahabu.
Ameongeza kuwa, lengo lingine la BOT ni kuhifadhi dhahabu kwenye benki kwa mujibu wa sheria ya madini kifungu cha 59 sura ya 123 ambacho kinaelekeza kila mwenye leseni ya uchimbaji na mchimbaji auze angalau asilimia 20 ya dhahabu anayoipeleka sokoni.
“Mheshimiwa waziri mkuu anayeiuzia benki kuu anapata punguzo la malipo katika mrahaba wake ambapo awali ilikuwa asilimia 6 lakini imepunguzwa hadi asilimia 4 na malipo ya ada yamepunguzwa kutoka asilimai 1 na kuwa 0 ,lakini hatumzuii mchimbaji kuuza asilimia 100 ya mziko wake” alisema Rehema.
Awali Vicky Msina meneja wa mawasiliano BOT alimweleza waziri mkuu kwamba, lengo la kushiriki maonyesho hayo ni kutoa elimu kwa wananchi kuwa benki kuu ni mdau wa wachimbaji wa madini ikiwemo dhahabu.
“Mbali na kununua dhahabu BOT inahifadhi fedha za kigeni kwa kutumia nyenzo mbalimbali moja wapo kununu dhahabu ili serikali iweze kupata fedha za kigeni na kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi” alisema Vicky.
Akiwa katika banda hilo waziri mkuu Majaliwa aliwapongeza BOT kwa kuweka mkakati imara kuhifadhi dhahabu ambapo hapo baadaye itasaidia nchi kwa manufaa ya wananche wake.
Waziri mkuu aliwasili jana mkoani Geita kufungua maonyesho ya 8 ya kitaifa ya teknolojia ya madini yaliyoanza septemba 18 na yanatarajiwa kuhitimishwa septemba 28,mwaka huu.

Comments
Post a Comment