MWANAUME AUWA MKEWE KWA KIPIGO AKILAZIMISHA APEWE FEDHA ZA MKOPO

Na, Ernest Magashi

Mwanamke mmoja aitwaye Manila Kiselya (48), mkazi wa Kitongoji cha Majengo, Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, amefariki dunia baada ya kupigwa na mumewe, John Kiganga, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni ugomvi uliotokana na fedha za mkopo ambazo mwanamke huyo alikopa kwa ajili ya kuongeza mtaji wa biashara yake.Tukio hilo la kusikitisha limetokea usiku wa kuamkia Julai 23, 2025, katika makazi yake, ambapo inadaiwa kuwa mume huyo alimshambulia mkewe kwa kipigo kikali hadi kupoteza maisha.Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majengo, Elizabeth Mwenda, ambaye alikuwepo eneo la tukio, alisema kuwa marehemu alikuwa amekopa fedha kutoka taasisi moja ya kifedha (jina halijajulikana) kwa lengo la kuendeleza biashara yake. 

Hata hivyo, mume wake alitaka fedha hizo, jambo lililosababisha ugomvi mkubwa uliomalizika kwa mauaji.“Elimu ya ulinzi wa wanawake inahitajika. Mwanamke huyu haikuwa mara ya kwanza kupigwa, lakini alikuwa anakataa kutoa taarifa kwa viongozi. Sasa tumepoteza mtu kwa sababu ya ukimya,” alisema Elizabeth.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wanawake wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia kutoa taarifa mapema kwa viongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi kwa vyombo vya usalama ili waweze kusaidiwa.Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bukombe, Haruni Kasubi, alifika katika eneo la tukio na kutoa elimu kwa wananchi, akisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba hakuna sababu yoyote ya mtu kumpiga au kumdhuru mwenzake.“Jamii isikubali mazoea ya ukatili. 

Majirani walikuwa wanasikia kelele, lakini hakuna aliyeripoti kwa balozi au kutoa msaada,tunatoa elimu mara kwa mara juu ya haki za wanawake, lakini bado jamii haitoi taarifa.

 Tunawahimiza watu kufika katika Dawati la Jinsia ili wapewe Elimu ya kuishi zaidi,” alisema mkuu wa Polisi  kasubiKwa upande Yohana Pius, ambaye ni mkazi wa eneo hilo ameeleza kuwa tukio hilo ni la kushtua kwani ni mara nyingi amekuwa akisikia mtu amepigwa na kupoteza maisha kwa kisa cha mapenzi na siyo kisa cha mkopo, hii ni Mpya kusikia kwa mwanandoa kuuawa kwa sababu ya fedha za mkopo .

 Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alitoroka baada ya tukio, akiwa na pikipiki yake na kuchukua fedha hizo za mkopo kiasi cha shilingi milioni 3.

 Juhudi za Polisi kumsaka zinaendelea na wametoa wito kwa jamii kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea.Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kwa uchunguzi na taratibu zaidi zinaendelea. "Wakati marehemu anapigwa, watoto walikuwa wakitazama runinga huku wakichukulia hali hiyo kama jambo la kawaida, ambapo Mara kwa Mara hutokea hali hiyo ikiwa ni ya kawaidi kwa wanandoa hao, onyo kwa jamii kubadilika na kutoa taarifa mapema kabla hali haijawa mbaya zaidi," alisema Mkuu wa Polisi  kasubi.

 Adha Mkuu wa Polisi Kasubi alitoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za mharifu  ili akamatwe na kufikishwa mbele ya sheria. 


 

Comments