SERIKALI INAENDELEA KUTEKELEZA MIRADI YA UMEME KWENYE MAENEO YA KIMKAKATI

 


Na, Ernest Magashi

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye  maeneo ya kimkakati nchini ikiwemo maeneo ya migodi midogo,  maeneo ya uvuvi, Viwanda na  maeneo ya shughuli za kiuchumi.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 14, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Mwibara, Mhe. Charles Kaijage aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali kupelekea umeme maeneo ya uvuvi ili kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
"Mheshimiwa Naibu Spika Mradi huu wa kupeleka umeme maeneo ya kimkakati umefikia zaidi ya maeneo 300 ikiwemo vituo vya afya na visima vya maji kwa maeneo ambayo yanatoa huduma za kijamii", amesema  Kapinga. 

Akijibu swali la Mbunge wa Igunga, Mhe. Nicholas Ngassa aliyeuliza lini Serikali itaanza usambazaji umeme kwenye Vitongoji vya Jimbo la Igunga. 

Mhe. Kapinga  alijibu nakusema  Jimbo la Igunga lina jumla ya Vitongoji 337 ambapo kati ya hivyo, Vitongoji 95 vimepatiwa umeme na katika Vitongoji 15 wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa miradi kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini awamu ya Pili A (HEP IIA) na Vitongoji 69 zabuni imetangazwa kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB).

Mhe, Kapinga mesema kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kutenga fedha za kuvipelekea umeme vitongoji 158 vilivyosalia.

Pia amekumbusha kuwa, gharama ya kuunganisha umeme kwa maeneo ya Vijijini ni sh27,000 na kuongeza kuwa, kuna mradi utakaoanza hivi karibuni unaohusisha Vitongoji ambavyo havina laini kubwa ya umeme na vilivyo na kwenye laini kubwa ya umeme.

Comments