MAJALIWA ACHAGIZA SIKU YA TANZANIA MAONESHO YA EXPO 2025, JAPAN



Na, Ernest Magashi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara kati ya Tanzania na Japan kutoka dola za kimarekani sh 7 bilioni mwaka 2020, hadi kufikia dola za kimarekani sh37 bilioni mwaka 2024 na hivyo kukuza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye nyanja za kiuchumi.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo 25 Mei, 2025 jijini Osaka  Japan wakati akimwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye maadhimisho ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Osaka Expo 2025 yanayoendelea nchini Japan, amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji  kwenye miradi ya Jotoardhi, Uchumi wa buluu, Afya, Elimu, Miundombinu, Kilimo, na Mifugo.
Mhe Majaliwa ametumia fursa ya siku ya Tanzania kuyaalika kampuni za Japan kuwekeza nchini pamoja na kushiriki kwenye maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama sabasaba ambayo hufanyika kuanzia  mwishoni mwa mwezi  juni.

‘’ Nipende kuwakaribisha wenzetu wa Japan kuja kuwekeza Tanzania kwani mazingira ya uwekezaji ni mazuri ‘’ Amesema Waziri Mkuu Majaliwa. 

Siku ya Tanzania kwenye maonesho ya Osaka Expo 2025 nchini Japan ilipambwa na ngoma za utamaduni na Taarabu asilia kutoka Zanzibar na kuhudhuriwa pia na Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa taasisi mbalimbali sambamba na maonesho ya Wiki ya Miundombinu  ya Osaka Expo 2025  yanayoendelea nchini Japan.

Comments