SERIKALI IMEAHIDI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Serikali imeahidi kuendelea kuboresha huduma za Afya nchini katika ngazi zote ili kila Mtanzania apate huduma za Afya Bora.

Hayo yamesemwa Aprili, 25, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa kwenye ziara yake Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha ambapo amesema kuwa lengo la uwekezaji katika sekta ya afya ni kusogeza huduma za afya kwa wananchi wote wa tanzania.
Dkt. Biteko amesema Serikali inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea na uwekezaji mkubwa wa kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini.


Akizungumza baada kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Meru, iliyopo Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, Mhe. Dkt. Biteko amesema lengo la uwekezaji katika sekta ya afya nikusigeza huduma za afya kwa Watanzania.
“ Kama mnavyofahamu afya ndio mtaji wa wananchi na Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga hospitali mpya na kufanyia ukarabati wa miundombinu,” amesema Dkt. Biteko.

Aliongeza kusema “ Watu wote nilioongea nao hapa hospitalini wamesema hali ya utoaji huduma imeimarika na ni nzuri, nataka niwaambie Rais Samia katika uongozi wake ameapa kuboresha hali za maisha ya Watanzania. Hapo awali ilimlazimu mgonjwa kutoa makozi siku tatu mfululizo ili kumfanyia kipimo cha ugonjwa wa kifua kikuu, leo tuna mashine ya kisasa inayotumia saa mbili kupata majibu ya mgonjwa,” amesema Dkt. Biteko. 


Ameendelea kusema ujenzi  na maboresho yaliyofanyika hospitalini hapo  imetumia raslimali za ndani (force account) na kazi imefanyika kwa ubora na kuzingatia thamani ya fedha.

Ameongeza kuwa katika kuelekea miaka 61 ya Muungano uwepo wa hospitali hiyo ni kiashiria cha kuwa nchi inapiga hatua kimaendeleo. Hivyo, wananchi hawana budi kuuenzi na kuutunza Muungano.

Dkt. Biteko amewataka wagonjwa kuwa wavumilivu wanapoenda kupata matibabu huku wakizingatia kuwa wahudumu wa afya wanafanya jitihada kubwa kuwapa huduma bora.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema kuwa wananchi wa eneo hilo wanafurahia huduma nzuri zinazotolewa na sasa idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa imeongezeka kutika 3,000 hadi wagojwa 12,000.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Meru, Daktari Elisante Fabiani amesema kuwa uboreshaji wa majengo katika hospitali hiyo umesaidia utoaji huduma na kuongeza idadi ya vipimo vya maabara kutoka 18 hadi 32.


“ Tuna mashine ya kisasa ya kupimia vimelea vya kifua kikuu na ndani ya saa mbili pekee mgonjwa anapata majibu ya kifua kikuu na kuanza matibabu na ina uwezo wa kugundua dawa ya kutumia,” ameeleza Daktari Fabian.

Dkt. Biteko amehitimisha ziara yake ya siku tano mkoani humo ambapo ametembelea Wilaya za Longido na Monduli ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 

Comments