Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amewafukuza watumishi wa kampuni ya uchimbaji wa madini mkoa wa Geita GGML akiwemo mwanasheria kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa RCC baada ya kutokuridhishwa na majibu yao kuhusu kiasi cha bilioni 9 za uwajibikaji kwa jamii CSR ambazo hazikutolewa kwa mwaka wa 2024.
Majibu kutoka kampuni ya GGML yameeleza kuwa, walishindwa kutoa fedha hiyo kutokana na halmashauri kutokuthibitisha mpango wa fedha hizo kwa wakati hivyo wakaamua kufuta mpango huo na kuuweka kuwa mpango wa mwaka mwingine wa 2025.
Mkuu wa mkoa Shigela alisema kitu hicho hakiwezekani, na ilitakiwa fedha hiyo itumike kwenye miradi ya mwaka mwingine badala ya kufutwa.
Shigela aliwafukuza watumishi hao na kuongeza kuwa hayupo tayari kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo mpaka pale watakapotoa pesa hiyo kama sheria inavyowataka labda waende TAMISEMI au madini au mahali pengine.
Hata hivyo watumishi hao waliondoka pasipo kutoa kauli yoyote na Mkuu wa mkoa kufunga mjadala wa kuhusu CSR huku wajumbe wa kikao wakipongeza uamuzi huo.
Comments
Post a Comment