Watanzania wamekumbushwa na kuendelea kuliombe Taifa la Tanzania.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema hayo leo Februari 16, 2025 wakati akishiriki ibada katika Kanisa la Africa Inland Church Chang’ombe jijini Dar es salaam.
Dkt. Biteko amesema Watanzania wanatakiea kuendelea kuiombea nchi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“ Tuendelee kuliombea kanisa, tuendelee kuiombea nchi yetu na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae kwa kweli anafanya kazi nzuri na sisi tunaofanya kazi karibu naye tunaona,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amewahimiza watanzania kudumisha upendo na amani nyakati zote hususani kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, ili uchaguzi huo usiwe sababu ya kuligawa Taifa na tofauti ya mitazamo.
“ Mungu ametupa bahati ya kuwa na nchi yenye amani, sisi tuilinde kwa wivu mkubwa kwa kuwa amani ikiondoka gharama yake ni kubwa" "Tuziombee pia nchi jirani zenye matatizo kwa vile tatizo la jirani linaweza kuwa tatizo lako wakati wowote ule, mfano mnakumbuka janga la covid 19 lilivyotuathiri dunia nzima,”amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha mipango na sera mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya dunia, ametolea mfano mabadiliko yaliyofanyika katika Sera ya Elimu.
“ Tunatengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo tulizunguka nchi nzima kwa ajili ya kukusanya maoni ya watu katika makundi mbalimbali ili tuweze kupata Tanzania tunayoitaka miaka 25 ijayo,” aliongeza Dkt. Biteko.
Mchungaji Dkt. Joseph Mayala Mitinje amewaasa waumini wa Kanisa hilo kukumbuka kufanya maombi na kusema kuwa ibada hiyo ilikuwa maalum kwa ajili kuiombea Serikali pamoja na mahitaji mbalimbali.
“Ili umtumie Mungu vizuri una mahitaji ya kila eneo hivyo asubuhi ya leo tunaombea mahitaji yetu kwa Bwana,” amesema Mchungaji Mitinje.
Mchungaji Dkt. Joseph ameahidi kuendelea kuliombea Taifa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali katika kutekeleza majukumu yao na Mungu aibariki Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani, umoja na mshikamano.
Naye, Mchungaji Andrew Chad kutoka nchini Uingereza akihubiri katika ibada hiyo amesema makanisa ya Uingereza na Tanzania yamekuwa na ushirikiano wa karibu na hivyo imeendelea kumpa fursa ya kuhubiri injili nchini.
Ambapo ameeleza kuwa alipokuja nchini alianza kuhubiri injili katika Kanisa la AICT Mpanda mkoani Rukwa kwa muda wa miaka nane.
Baadaye yeye na wenzake walianzisha makanisa mengi katika maeneo mbalimbali ikiwemo mkoani Tanga ambapo alihudumu kwa muda wa miaka sita.
“ Tulipata wito kwenda mkoani Tanga kuhubiri injili kwa upande wa watu wa kabila la Wadigo na kuwafundisha watu wanampenda Mungu,” amesema Mchungaji Chad.
Ameongeza kuwa Mungu anaweza kumtumia binadamu yeyote kwa utukufu wake, sambamba na kuwaasa wakristo kuishi kwa upendo na kuwa wakarimu kwa watu wote.
Comments
Post a Comment