Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewasili jana nchini India kwa ajili ya kushiriki mikutano mbalimbali ya kimataifa ya nishati ambayo inaenda sambamba na Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Nishati ya India mwaka 2025 (India 3rd Annual Energy Week) kuanzia tarehe 11 hadi 14 Februari, 2025.
Katika Uwanja wa Kimataifa wa India Gandhi, jijini New Delhi, Dkt.Biteko amepokelewa na mwenyeji wake Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta na Gesi India, Sandeep Jain.
Imedaiwa kuwa Wiki ya Nishati India itakutanisha Mawaziri na Watendaji Wakuu wa Sekta ya Nishati kutoka maeneo mbalimbali duniani, watunga sera na wavumbuzi wa teknolojia mbalimbali za kisasa za nishati kwa lengo la kuja na mustakabali endelevu wa upatikanaji nishati.
Pia, Wiki hiyo itahusisha pia maonesho ya teknolojia mbalimbali za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Dkt.Biteko ameambatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakiongozwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga.
Comments
Post a Comment