WATANZANIA KUNUFAIKA NA MASHINDANO YA CHAN 2025, AFCON 2027

 


đź“ŚMashindano yameipa heshima Tanzania kimataifa


đź“ŚRais Samia kinara wa Michezo nchini


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Watanzania watanufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitakazopatikana kuelekea mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.



Hayo yamebainishwa leo Januari 15, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Michezo kuelekea CHAN 2025 na AFCON 2027 jijini Dar es Salaam. 


"Nchi yetu imepata heshima kubwa kimataifa na hii haiji kwa bahati mbaya imesababishwa na ukuaji wa demokrasia iliyojengwa na Rais Samia kwenye mataifa mbalimbali duniani, " amesema Dkt. Biteko.


Aidha, Dkt. Biteko amewapongeza wadau wa michezo waliotoa mawazo ya kuanzishwa kwa kongamano hilo ili kutangaziana fursa zitakazotokea wakati wa mashindano hayo. 


Ameeleza kuwa, mashindano yatawakutanisha wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali na kuna wajibu wa kufanya maandalizi kwa ufanisi mkubwa ili kunufaika na mashindano kupitia fursa mbalimbali za usafirishaji, malazi na burudani. 



"Fursa za mashindano haya zitakuza uchumi wa nchi yetu na kufanya vikundi vya watu au kampuni mbalimbali kufanya biashara na kukuza uchumi wao na hatimaye kuondoa umaskini miongoni mwetu, " ameongeza Dkt. Biteko. 


Vile vile, Dkt. Biteko amempongeza Rais Samia kwa kuwa kinara wa kuhamasisha ushiriki wa watanzania katika sekta ya michezo ili vijana kukuza uchumi wao. 


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwijuma amesema lengo la kongamano ni kupokea maoni ya wadau mbalimbali na kuchanganua fursa zitakazokuja pamoja kuelekea mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027 ambazo watanzania watanufaika nazo.


Mashindano ya CHAN 2025 yanatarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu na AFCON yamepangwa kufanyika mwaka 2027.

Comments