DKT KAZUNGU ASHIRIKI HAFLA YA UFUNGUZI WA WIKI YA UENDELEZAJI WA NISHATI NA UTOAJI WA TUZO ZA UMAHIRI ABU DHABI



 *DKT KAZUNGU ATETA NA BALOZI WA TANZANIA ABU DHABI*



📌 *Anadi miradi ya nishati kuvutia wawekezaji kutoka Abu Dhabi*


📌 *Ashiriki hafla ya ufunguzi wa Wiki ya uendelezaji Nishati Abu Dhabi na utoaji tuzo za umahiri*


📌 *Balozi wa Tanzania Abu Dhabi awataka watanzania kuchangamkia fursa za ajira*



Abu Dhabi, UAE



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia umeme na nishati jadidifu Dkt Khatibu Kazungu amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania Abu Dhabi Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed alipokwenda kwenye ofisi za ubalozi huo kumtembelea.


Dkt Kazungu aliambatana na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Baraza la 15 la Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu IRENA mjini Abu Dhabi anbapo alimweleza Balozi Yacoub umuhimu wa Tanzania kupata fedha za kutosha kutoka kwa wawekezaji ili iweze kutekeleza miradi ya nishati jadidifu anbayo ni rafiki kwa mazingira na kuepuka athari za mabadiliko ya Tabianchi.


‘’ Tunaishukuru sana Serikali ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri inayofanya kutoa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi na sisi kama Wizara ya Nishati tunaahidi kutekeleza kwa vitendo." Alisema Dkt Kazungu


Awali akizungumza kwenye kikao hicho Balozi wa Tanzania, Abu dhabi Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed alisema, Watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa za ajira zilizopo mjini Abu Dhabi kama ilivyo kwa nchi nyingine kama India, Kenya na Uganda ili kuinua uchumi wa nchi na kukuza kipato kwa wananchi wake


Aliipongeza Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha umeme unakuwepo wa kutosha na wa uhakika hususani kwenye mradi wa treni ya mwendo kasi ambayo umekuwa na tija kwa wananchi na Serikali kwa ujumla


‘’ Nitoe rai kwa Watanzania kuwa mabalozi wazuri wa mradi huu wa treni ya SGR pamoja na wataalamu wa TRC na TANESCO kuhakikisha wanafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha hakuna hitilafu yoyote na watanzania wafurahie matunda ya mradi huo kutoka kwenye Serikali yao.


Katika hatua nyingine Dkt. Kazungu alishiriki hafla ya ufunguzi wa wiki ya uendelezaji nishati ikiwa ni mwendelezo wa fursa zilizopo kwenye Baraza Kuu la 15 la IRENA ili kutoa fursa za kubadilishana uzoefu na wawekezaji kwenye maonesho hayo.



Hafla hiyo iliambatana na utoaji wa tuzo za Rais wa umoja wa falme za kiarabu UAE zijulikanazo kama Zayed Sustainability Prize, kutambua mchango wa makundi mbalimbali yanayoleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya nishati ambapo mtanzania kutoka taasisi ya Open Map Development ameshinda kwenye kipengele cha mabadiliko ya tabianchi.

Comments