Na, Ernest Magashi
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa pia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024, CCM imedhamiria kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ili kubadilisha hali za maisha ya wananchi.
Amesema Kata ya Namonge ni kati ya kata 17 zinazounda Wilaya ya Bukombe yenye vijiji vinane na vitongoji 36 ambayo imeendelea kupiga hatua ya kimaendeleo kwa kuwa na mtandao mrefu zaidi wa barabara kuliko kata zingine.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 25, 2024 wakati akihutubia na kuwanadi wagombea kwenye mkutano wa Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wilayani Bukombe zilizofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Namonge kata ya Namonge Tarafa ya Siloka Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
“ Tunataka maendeleo kwa ajili ya watu wetu na kata hii imeandikisha idadi kubwa ya wananchi leo nimekuja kuwaomba mchague viongozi wa CCM ili tuendeleze jitihada zetu za kuwaletea maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kata hiyo kuwa ni ujenzi wa shule tatu za sekondari, zahanati nne na kituo cha afya kimoja.
“ Awali tulikuwa na barabara kutoka Uyovu hadi Namonge na barabara ya kwenda maeneo mengine haikuwa nzuri, barabara ya kutoka Namonge hadi Mjimwema haikuwepo", " leo tumekuja na kazi moja ya kuomba kura zenu wananchi wa Namonge,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Alielezea mipango ya maendeleo ya baadae kuwa ni kujenga shule ya sekondari na kuimarisha hospitali ili iweze kutoa huduma za upasuaji katika kata hiyo.
Dkt. Biteko amesema ili kufanya kazi vizuri zaidi ni vyema kupata viongozi wa vijiji na vitongoji wanaotokana na chama kimoja cha CCM kwa vile wanauhusiano mzuri wa kazi haliambayo itarahisisha juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi.
Dkt. Biteko amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Bukombe na Watanzania wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi na kupiga kura ili kuchagua viongozi wao Novemba 27,2024.
“ Tunatambua uchaguzi huu ni muhimu na sisi tunausimamia kwa haki ili kupata viongozi watakaotatua shida za wananchi,” aliongezaDkt. Biteko.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja amesema itakapofika siku ya kupiga kura Novemba 27, 2024 wananchi wa Bukombe wajitokeze kwa wingi ili kutimiza haki yao ya kikatiba ili kupata viongozi bora kupitia CCM.
Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini zitahitimishwa Novemba 26, 2024 na mkoani Geita mkutano wa hadhara wa kampeni hizo utafanyika Kata ya Uyovu Tarafa ya Siloka Wilayani Bukombe ambapo Dkt. Biteko atakuwa mgeni rasmi.
Comments
Post a Comment