Wananchi waishukuru Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwani Wagombea wa CCM waliahidi upatikani wa maji katika maeneo hayo wakati wa kampeni 2020.
Mradi wa maji uliotekelezwa katika kata ya Runzewe Magharibi na kughalimu Tsh. Milioni 954 sasa umeanza kutoa huduma baada ya mkandarasi YAJUKI INVESTMENT COMPANY LIMITED kuukamilisha hali iliyomfanya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bukombe Eng. James Benny kuelekeza mradi huu uanze kutoa huduma.
Mradi huu wenye mtandao wa bomba jumla ya Kilomita 16 na vituo 12 vya kuchotea maji, utawanufaisha wakazi wapatao 11,960 katika vijiji vya Namsega, Kazilamuyaye na Msangila kama alivyoeleza Mhandisi James.
Akizungumza kwa niaba ya watumiaji wa huduma, Chausiku Ally ambaye ni mkazi wa kijiji cha Namsega amesema anaishukuru serikali kwa kuendelea kusogeza huduma kwa wananchi na kueleza furaha yao juu ya upatikanaji wa maji kwani kutawapunguzia adha kubwa waliyokuwa nayo.
Naye diwani wa kata hii Mheshimiwa John Nguhi amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt. Doto Biteko kwa kufuatilia ahadi hii ambayo aliitoa kwenye mkutano wa kampeni alipokuwa kijiji cha Kazilamuyaye mwaka 2020 ambayo Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kuleta fedha kwa utekelezaji wake.
Comments
Post a Comment