MATUKIO MATATU YA KIKATILI YATIKISA BUKOMBE

 Mtoto wa miezi minne auawa na kunyofolewa viungo


Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya Bukombe, Deograsia Mkapa

Na Henry Evarist, Bukombe

Mtoto mchanga wa miezi minne mwili wake umeokotwa katika kata ya Katome wilayani Bukombe ukiwa umeondolewa mkono na mguu katika mwendelezo wa matukio ya ukatili Julai 25, 2024.

Mwili huo umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ambapo bado jina na wazazi wake bado hawajajulikana ambapo mganga mkuu wa wilaya hiyo (DMO) Deograsia Mkapa alisema mtoto huyo aliyeuawa na wasiojulikana, hana ualbino.

Kufuatia tukio hilo ambalo polisi mkoa wa Geita wamesema uchunguzi bado unaendelea, Dkt. Deograsia aliwataka wazazi na jamii kuchukua hatua za kuwalinda watoto

“Matukio haya siyo hapa Bukombe tu. Matukio yamekuwa mengi kama ambavyo tumekuwa tukiona yanaripotiwa kwenye vyombo vya habaria katika maeneo mengine ya nchi. Hivyo natoa wito kwa wanawake kuwalinda wanawake na watoto” alisema Dkt. Deograsia



Rehema Paul akiwa hospitali ya wilaya Bukombe napoendelea kupatiwa matibabu

Tukio lingine ni mwanamke Rehema Paul (26) aliyenusurika kuuawa kwa kukatwa na mapanga katika maeneo mbalimbali ya mwili wake katika eneo la Mnada wa Zamani maarufu kama “Masankuloni” majira ya saa mbili za usiku alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwa wifi yake mtaa wa Kapela jirani na anapoishi.

Kiganja cha mkono wa kulia wa Rehema kimehifadhiwa pia chumba cha maiti baada ya kuondolewa wakati akijikinga na shambulio kichwani huku mkono wa kushoto na maeneo ya kichwani yakiwa yamejeruhiwa vibaya.

Dada yake Rehema aliyejitambulisha kwa jina la Gaudensia George aliyekutwa wodini hapo akimuuguza ndugu yake pamoja na kupongeza jitihada za hospitali ya wilaya katika kunusuru maisha ya ndugu

Aidha, Mwenyekiti wa kitongoji cha Igulwa Kata ya Igulwa, Lucy Samweli alisema kuwa alipigiwa simu majira ya saa mbili za usiku na kuelezwa kuwa Rehema amekatwa na kitu chenye ncha kali ambapo alifika na kupiga simu polisi ambao walifika haraka na kumuwaisha hospitali ya wilaya.

“Kufuatia tukio hili la kusikitisha natoa wito wito kwa wananchi wangu tujilinde sisi kwa sisi” alisema Lucy na kuongeza kuwa mpaka sasa watu wane tayari wamekamatwa kufutia tukio hilo.

Jirani wa majeruhi, Joyce Selenda ameeleza kusikitishwa na tukio hilo kwa kuwa jirani yake Rehema wa kwa mama Esther alikuwa ni mtu aliyeishi vizuri na majirani.

Katibu tawala wilaya ya Bukombe, Ally Mketo akimjulia khali Rehema Paul hospitalini akiwa ameambatana na mganga mkuu wa halmashauri hiyo, Dkt. Deograsia Mkapa

Hata hivyo, Rehema leo amaeweza kuzungumza na mwandishi wa Bukombe sasa na kusimulia tukio zima lilivyokuwa akitaja sababu na watu anaohisi kuhusika (majina yao tunayahifadhi kwa sababu za maalumu) huku deni la kiasi cha shilingi 10,000 na wivu wa mapenzi vikihisiwa.

Tukio la tatu linahusu mtu mmoja anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 30-35 ambaye jina lake halikuweza kutambulika mara moja mwili wake umeokotwa jirani na hospitali ya wilaya ya Bukombe ukiwa tayari umeanza kuharibika.


Maafisa wa polisi wilaya ya Bukombe wakichukua mwili wa marehemu kwa uchunguzi na kuuhifadhi

Taarifa za kuonekana kwa mwili huo wa mtu ambaye ametambuliwa kuwa na matatizo ya akili (chizi) zilipatikana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika hospitalini hapo yakiongozwa na katibu tawala wa wilaya kwa niaba ya mkuu wa wilaya ambao walifika eneo hilo na mwili kuchukuliwa na polisi na kuhifadhiwa hospitali ya wilaya.

Mganga mkuu alidhibitisha kupokea miili hiyo ambayo ambayo tayari imehifadhiwa mochwari na kusema kuwa mwili wa mtu mzima aliyeokotwa umetambuliwa kwani ni mtu ambaye alikuwa akipatiwa matibabu ya matatizo ya akili mara kwa mara hospitalini hapo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Sofia Jongo alipopigiwa simu kuthibitisha kutokea kwa matukio hayo
simu yake iliita bila majibu.

Wananchi waliozungumza na Bukombe sasa wamelitaka jeshi la polisi kuwatafuta na kuwachukulia hatua kali watakaobainika kuhusika katika matukio hayo ya kikatili. 



Comments