KATIBU TAWALA BUKOMBE AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA MASHUJAA.

 

Katibu tawala wa wilaya Bukombe, Aly Mketo (mwenye trakisuti na glavuzi) akiongoza wananchi wa wilaya hiyo kufanya usafi katika hospitali ya wilaya ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Julai 25, 2024

Na Henry Evarist

Katibu tawala wa wilaya Bukombe, Aly Mketo ameongoza maadhimisho ya siku ya mashujaa kwa kufanya usafi hospitali ya wilaya pamoja na mazoezi ya viungo.

Akiongoza kamati ya ulinzi na usalama, wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri pamoja na viongozi wengine mapema leo Julai 25, Mketo kwaniaba ya mkuu wa wilaya hiyo, Mhandisi Paskas Muragili aliwataka wananchi wote kuwaenzi mashujaa waliopigania uhuru kwa kufanya matukio mbalimbali ikiwemo usafi na utunzaji wa mazingira pamoja na kuwaombea waliotangulia mbele ya haki.

"Lengo la siku hii ni kuwakumbuka wapambanaji wetu waliomwaga damu nyingi kwa ajili ya kudai uhuru wakiwemo Mwalimu Nyerere na Karume. Katika harakati za kudai uhuru mashujaa wetu baadhi walimwaga damu wakipigania taifa ili ikiwemo vita ya majimaji, hivyo lazima tuwaenzi na kila mmoja kwa Imani yake kuwaombea dua na maombi" alisema Mketo


 
Katibu tawala wa wilaya Bukombe, Aly Mketo (katikati) akizungumza na watumishi wa wilaya ya Bukombe (Hawapo pichani) baada ya kumaliza kufanya usafi na mazoezi katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Julai 25, 2024 katika hospitali ya wilaya

Aidha aliwataka vijana na watu mbalimbali kuwa na moyo wa uzalendo pamoja na kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya usalama ya wilaya ya Bukombe ambaye pia ni mkufunzi wa Jeshi la Akiba, Staff Sargent Juma Magembe aliwataka vijana kujiunga kwa wingi katika jeshi hilo ili kutoa mchango wao kwa taifa

Mganga Mkuu wa halmashauri ya Bukombe, Dkt. Gaudensia Mkapa aliwashukuru wote walishiriki katika usafi wa hospitali ya wilaya akisema ni upendo mkubwa kwa wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo kuwa imewaongezea morali wa kufanyakazi.

Wakizungumzia maadhimisho hayo, wananchi waumepongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa kuadhimisha siku hiyo muhimu

"Vijana wanapoona matukio kama haya inawatia moyo na kuona kuwa taifa hili wapo waliolipigania na hivyo nao kuvutiwa na kuwa tayari kutumika kwa faida ya wengine" alisema Hussein Masanja mkazi wa kata ya Katente

Baadhi ya Vijana wilayani Bukombe wakishiriki zoezi la usafi wa mazingira katika hospitali ya wilaya katika kuadhimisha Siku ya Mashujaa Julai 25, 2025

Naye kijana Juma Mstapha kutoka kata ya Igulwa alieza kuvutiwa na maadhimisho hayo akiahidi mwakani kushiriki kimamilifu.

“Hii ni heshima kwa mashujaa wa taifa hili na kila kijana angetamani kuwa historia ya nchi yake hivyo hata kushiriki matukio kama usafi katika maeneo ya umma na kusikiliza hotuba mbalimbali za viongozi ni jambo linazidi kunipa hamasa ya kutumikia taifa langu Tanzania” alimalizia Juma katika mahojiano na mwandishi wa habari hii.




Comments