HONGERENI HALMASHAURI YA WILAYA YA BUKOMBE KWA KUPATA HATI SAFI- RC SHIGELA







Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa kupata hati safi kutokana na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.


Shigela ameyasema hayo tarehe 24 Juni, 2024 wakati wa mkutano maalum wa kujadili taarifa ya utekelezaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2022/2023 uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.


“Niwapongeze sana kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa fedha, hii inaonesha ukomavu mkubwa sana katika utendaji wenu”.


Vilevile Shigela amewataka watendaji wote wa Halmashauri kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha hakuna mapato yanayopotea.



Aidha Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe Paskasi Muragili amesema kuwa ili Bukombe iendelee kuwa na hati safi, kila mmoja anatakiwa kuzingatia sheria na miongozo katika utendaji kazi.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe Mhe. Yusuph Mohamed amesema kuwa hadi sasa Halmashauri imefanikiwa kukusanya asilimia 91 ya mapato na amewataka wataalam kuongeza kasi ili kufikia asilimia 100.


Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa, Wilaya, wajumbe wa kamati ya Usalama pamoja na wakuu wa Idara na vitengo.     

                  

Comments