Bukombe waadhimisha siku ya Familia Duniani 2024

Wanakijiji cha Silamila kata ya Butinzya wilayani Bukombe wakiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani Mei 15, 2024

Na Henry Evarist 

Leo, Halmashauri ya wilaya ya Bukombe wameadhimisha siku ya familia duniani kwa kuwataka wanafamilia kuchukuliana katika mapungufu yao kwa faida ya watoto na taifa kwa ujumla 

Siku hiyo ambayo uadhimishwa duniani kote Mei 15 kila mwaka, kiwilaya imeadhimisha katika viwanja vya ofisi ya kijiji cha Silamila kata ya Butinzya ikiwa na kaulimbiu isemayo “Tukubali tofauti zetu kwenye familia, kuimarisha malezi ya watoto”

Akifafanua kaulimbiu hiyo katika risala iliyosomwa na Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Butinzya, Feruzi Shija alisema “Kaulimbiu hii inalenga kukuza ufahamu wa umuhimu wa familia katika kujenga jamii imara na kukuza mahusiano yenye afya kati ya wanafamilia”

 “Pia ni fursa ya kusherehekea na kutafakari juu ya majukumu, thamani, na mchango wa familia katika maisha yetu” alisema Shija

Shija aliongeza kuwa siku ya familia duniani imekuwa ikitoa fursa ya kuzingatia changamoto zinazokabili familia leo, kama vile mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, na kiutamaduni. 

“Inasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika familia ili kujenga jamii yenye ustawi na maendeleo endelevu. Ni wakati wa kushirikiana a kufanya kazi pamoja kuboresha mazingira ya familia na kuimarisha mahusiano ndani ya jamii” ni maneno ya kwenye risala.

Mgeni rasmi Diwani kata ya Butinzya, Amos Shimo akihutubia kwenye maadhimisho hayo

Mgeni rasmi katika siku hiyo ya familia 2024 alikuwa ni diwani wa kata ya Butinzya Mhe.Elias Shimo ambaye pamoja na mengine aliyekumbushia hadithi ya muujiza wa kwanza wa Yesu Kristu kwenye harusi huko Kana ya Galilaya akionesha utii kwa mzazi wake alimtaka aongeze vinywaji na Yesu kukubali kufanya hivyo alijua wakati ulikuwa haujafika

Mhe. Shimo alisisitiza watoto kuwa na utii kwa wazazi na walezi ili kuwa chanzo cha furaha katika familia akiwataka pia wazazi kuhakikisha wanawatimizia mahitaji yao ikiwemo chakula, elimu na mavazi.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Bukombe, Mellania Kwai alisema siku ya familia inapaswa kutumika kuwakumbusha wanafamilia umuhimu wa maadili mema na upendo miongoni mwao.

Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Bukombe, Mellania Kwai akimkaribisha mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani Mei 15, 2024 Silamila-Butinzya, Bukombe.

Mellania aligusia pia kaulimbiu kuwa inasisitiza upendo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima inayopelekea familia nyingi kusambaratika na kuacha watoto bila uangalizi wapamoja hivyo  kukosa huduma muhimu.

Maadhimisho hayo yalilenga pia  kuwakumbusha wazazi na walezi wajibu wao wa msingi katika malezi ya watoto na familia hasa akina baba wajibu wenu kama wazazi au walezi kwa watoto katika maeneo makuu matatu ya msingi 

“Kumjali mtoto katika mahitaji ya msingi, kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuzungumza na mtoto mara kwa mara ili kufahamu changamoto zinazomkabili na maendeleo yake kwa ujumla. ikiwa ni pamoja na kuwapatia muda wa kutosha” alisema Mellania.
Kila ifikapo Mei 15 ya kila mwaka tunaadhimisha siku ya familia duniani ikiwa ni utaratibu au kipindi cha kuadhimisha umuhimu wa familia katika jamii kwa kuwa na kauli mbiu mbalimbali.

Siku hiyo imetumika pia kuelezea mafanikio ya halmashauri ya wilaya ya Bukombe kupitia idara ya maendeleo ya jamii ambapo jumla ya wanachi 4682 wamejengewa uwezo katika masuala mbalimbali ya familia. Aidha jumla ya wanafunzi 5899 wa shule za msingi na sekondari Msonga, Doto Biteko, Uyovu na Bukombe wamepata elimu ya familia bora. Vilevile makundi mbalimbali kama vile bodaboda, wauza mbogamboga, wauza samaki, mama ntilie na kadharika wamefikiwa na elimu ya familia.

Msoma risala Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Butinzya, Feruz Shija 

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo kulielezwa kuwepo kwa matukio mengi ya ukatili wa watoto na wanawake yanayoshuhudiwa katika ngazi ya familia na katika jamii ya Bukombe. 

Maadhimisho hayo yalienda pamoja na zoezi la usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miezi mitatu na miaka mitano kutoka kwa msajili msaidizi ambaye pia ni Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Bukombe, Diana Beatus.
Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Bukombe, Diana Beatus akiendelea na zoezi la kusajili watoto na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa.

Katika hali ambayo haikutarajiwa, wananchi wa kijiji cha Silamila walionesha kufurahishwa na elimu ya UKIMWI iliyotolewa pamoja na zoezi la upimaji wa virus hivyo kutokana idadi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma hiyo jambo lililomwinua diwani wa kata hiyo kuomba mkutano wa hadhara utakaohusisha upimaji ili watu wote waweze kufikiwa na huduma hiyo
Muuguzi msaidizi, Aloyce Mwanashindano akitoa huduma ya ushauri, unasihi na upimaji wa virus vya ukimwi wakati wa maadhimisho ya siku ya familia Duniani Mei 15, 2024.

Matukio mengine yaliyoshudhudiwa katika maadhimisho hayo ni pamoja na elimu ya lishe ambapo ilielezwa kuwa mtoto anapokuwa chini ya umri wa miaka miwili anahitaji lishe bora ili juzuia udumavu.

“Ni rahisi kudhibiti udumavu au kuruhusu udumavu utokee katika umri huu pale inapokosekana lishe bora kwa mtoto” alisema afisa lishe wa wilaya, Eliud Mwakasinga

Mwakasinga aliyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na vyakaula kama mahindi, mchele, viazi, mihogo na mboga kama maziwa, nyama, mayai au maharage, dengu, mbegu za maboga pamoja na mbogambago kama mchicha, matunda na mafuta ya alzeti, pamba au karanga. 

Kwaya ya Mtakatifu Anthony wa Padua parokia ya Silamila- Butinzya

Comments