Sheikh wa wilaya ya Bukombe awataka watanzania kumuombea Dkt. Biteko


Sheikh wa wilaya na Imamu wa msikiti mkuu wa wilaya ya Bukombe, Ally Jumapili amewataka Waislamu wote na wasiokuwa waislamu kumuombea heri Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania na Waziri wa Nishati ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Doto Biteko ili azidi kuwatumikia watanzania na wananchi wa jimbo la Bukombe.


Sheikh Jumapili ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 10, 2024 wakati akiongoza swala ya Eid al- Fitr iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Igulwa iliyopo mjini Ushirombo wilayani Bukombe ambapo alitumia hadhara hiyo kuelezea wema wa Dkt. Biteko na kumpongeza kwa jinsi anavyowajali na kuwatumikia watanzania bila kujali itikadi za dini, vyama au maeneo wanayotoka


“Mbunge wetu Dkt. Biteko amekuwa mtu mwema sana na ambaye Mungu amemjaria upendo kwa watu wote. Wote tumekuwa mashuhuda kwa jinsi anavyojitoa bila kubagua dini, rangi wala kabila. Hivyo tumuombee Mungu amjalie kheri” alisema Sheikh Jumapili


Maneno hayo yaliungwa mkono na Sheikh Juma Milanzi aliyesimama na kuwataka waislamu waliohudhuria swala hiyo ya Eid kumuomba Mungu amlinde Dkt. Biteko na kumuona kuwa ni mwema kwa kuwa kweli ni mwema


“Mungu amlinde Doto Biteko na kumjalia kheri zile anazozitarajia na asizozitarajia kutokana na wema wake usio na shaka kwa watu wote wa Bukombe” alithibisha sheikh Milanzi




Akitoa salaam za mbunge, mwakilishi wa ofisi ya mbunge wa jimbo la Bukombe, Mwalimu Abdulmajid Yusuph alisema mbunge huyo anawapenda, anawatakia heri na anaahidi kuendelea kuwaunga mkono katika mambo yote yanayohusu imani na maendeleo ya wilaya ya Bukombe na Tanzania kwa ujumla.


“Tunaposherekea sikukuu hii ya Eid el fitr, tuna furaha kuona hata familia zenye mahitaji maalumu takribani 360 zimeweza kupatiwa msaada wa chakula na mbunge wetu Dkt. Biteko ili nao waweze kufurahia sikukuu hii kwa upendo na amani” alisema Mwl. Yusuph




Awali akitoa salaam za wilaya katika swala hiyo katibu tawala wa wilaya ya Bukombe, Ally Mketo aliwahakikishia wananchi na waislamu Wote kuwa ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya wilaya hiyo na hivyo kuwataka kusherekea bila hofu yoyote.


Aidha, Mketo alimpongeza mbunge wa jimbo hilo kuwa amekuwa mstari wa mbele katika kuinua elimu wilayani humo na kuwataka waislamu kutumia fursa hiyo ili kujiletea maendeo katika ngazi ya familia, wilaya na taifa kwa ujumla.


“ Wilaya yetu imepokea kiasi cha shilingi bilioni 2.2 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuboresha elimu ya sekondari ambapo madarasa mapya 72 na matundu ya vyoo 102 yanajengwa. Hii ni fedha nyingi hivyo ni lazima tumshukuru mbunge wetu kwa kutuwakilisha vyema na tumuombee Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan aendelee kumwamini na kuzidi kuwapenda watu wa Bukombe” alisema Mketo




Katika khotuba iliyotolewa viwanjani hapo na Hustadh Twaha Hassan Said alisisitiza waislamu kuitumia fursa ya elimu inayopiganiwa wilayani humo chini ya mbunge Dkt. Biteko ili kuepuka kubaki nyuma kwenye suala la maendeleo.


“Waislaam tusibaki nyuma katika mambo ya maendeleo. Jihadi yetu iwe ni ya maendeleo. Bado tunahitaji wataalamu wengi katika sekta mbalimbali na siyo jihadi ya kujilipua na mabomu sokoni bali jihadi yetu iwe kutumia shule hizi zinazojengwa kwa ajili ya kujiletea maendeleo yetu wenyewe, wilaya na taifa” alisema Hustadh Hassan




Eid al-Fitri ni siku kuu ya Kiislamu ya kusherehekea kumalizika kwa Mfungo wa Ramadhani. Mwezi wa Ramadhani ambao ndani yake imefaradhishwa funga ambayo imeambatanishwa na matendo mbali mbali ya sunnah, umekusudiwa uwe mwezi wa mafunzo na mazoezi ya kumfanya mja awe mchaji Mungu katika kiwango kinachostahiki kwa kipindi chote cha mwaka mzima.


Swala ya iko mara mbili - Eid al-Fitri na Iddil-Hajj (kilele cha ibada ya Hija) ni sunnah. Swala ya Eid inaswaliwa kwa rakaa mbili na kufuatiwa na Khutuba mbili kama zile zinazosomwa kabla ya swala ya Ijumaa. Swala ya eid ina Takbira 12,takbira 7 hutolewa katika rakaa ya kwanza kabla ya kusoma suratul-Faatiha na takbira 5 huletwa katika rakaa ya pili. 


Vile-vile kabla ya kusoma suratul-Faatiha.Mahali pa kuswalia eid panatakiwa kuwa uwanjani ili Waislamu wakusanyike pamoja kutoka sehemu mbali mbali za mji. Mtume (S.A.W) alikuwa akifanya hivyo. Ni sunnah kula chochote kabla ya kuswali Iddil-Fitri


Kitaifa swala ya Eid al-Fitri imeswaliwa katika msikiti wa Mohamed VI, uliopo Kinondoni, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mawaziri pamoja na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.


Katika swala hiyo ya kitaifa, Sheikh Mkuu, Abubakar Zubeir amesema sikukuu ya Idd El Fitri ni siku ya kutenda mambo mema na kushirikiana zaidi na sio siku ya kutenda maasi.


"Siku ya Idd el- Fitri ni siku ya furaha, kuitana kushirikiana na kumuomba Mungu msamaha zaidi, sio siku ya kumuasi Mungu" alisisitiza Sheikh Zubeir


Katika ibada hiyo ya Dar-es-Salaam, Sheikh Zubeir amewaomba Waislamu kujitokeza kwa wingi kuhudhuria Baraza la Eid litakalofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, litakalohudhuriwa na Rais Samia leo kuanzia saa 10 alasiri.

Baadhi ya Wananchi wa wilaya ya Bukombe wakishiriki swala ya Eid Al fitr katika viwanja vya Shule ya msingi Igulwa wilayani humo

Viongozi wa BAKWATA wilayani Bukombe wakiswali swala ya Eid Al fitri wilayani Jumatano Aprili 10,2024


Comments