KAZI ZITAKAZOTEKELEZWA NA WIZARA YA NISHATI KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25 KATIKA HOTUBA YA BAJETI ILIYOWASILISHWA BUNGENI NA NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI MHESHIMIWA DKT. DOTO MASHAKA BITEKO (MB), LEO APRILI 24, 2024



Miradi ya Kuzalisha Umeme


-Wizara imepanga kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia mradi wa Julius Nyerere (MW 2,115) ambapo kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo la mitambo (power house) na ufungaji wa mitambo saba (7) ya kuzalisha umeme ambayo kwa sasa ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.  


-Wizara pia itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi kwa kukamilisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilomita 19.2 kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi kwenda Gongolamboto hadi Mbagala Jijini Dar es Salaam na kufunga transfoma maeneo ya Gongolamboto na Mbagala. 



- Miradi mingine ya uzalishaji wa umeme itakayotekelezwa ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Malagarasi – MW 49.5; mradi wa kuzalisha umeme jua Shinyanga – MW 150; ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Hale; mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Kakono – MW 87.8; na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya mto Kikonge–MW 321. 


-Aidha, Serikali pia itaendelea kuelekeza nguvu katika uzalishaji wa umeme jotoardhi ambapo itakamilisha uchorongaji wa visima vitatu (3) vya uhakiki (exploratory wells) ili kuhakiki hifadhi, kiwango na ubora wa rasilimali ya jotoardhi katika mradi wa Ngozi (Mbeya) wenye uwezo wa kuzalisha MW 30 kwa awamu ya kwanza pamoja na kuanza ujenzi wa mtambo mdogo wa kuzalisha umeme (wellhead generator) wa MW 5. 


- Vilevile, Serikali itaanza utekelezaji wa programu ya uchorongaji wa visima vinne (4) vya uhakiki katika mradi la Kiejo Mbaka (Mbeya) wenye uwezo wa kuzalisha MW 60. 


Miradi ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme

 

- Miundombinu imara ya kusafirisha na kusambaza umeme ndiyo msingi thabiti wa kuwa na umeme wa uhakika. Hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika mwaka 2024/25 ni pamoja na kukamilisha mradi wa kusafirisha umeme kutoka Julius Nyerere Hydro Power Plant hadi Chalinze – Kilovoti 400 na Kituo cha Kupoza Umeme, Chalinze ambapo kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kumalizia kazi zilizobaki katika kituo cha kupoza umeme ikiwemo majengo, barabara, njia ya kusafirisha umeme na marekebisho mbalimbali. 


-Serikali itaendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya Chalinze na Dodoma. 


-Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha kusafirisha umeme unaotoka katika Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere kupitia Chalinze, kwenda mkoani Dodoma na kuusambaza katika mikoa mbalimbali nchini. 


- Miradi mingine ya usafirishaji wa umeme itakayotekelezwa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze - Kinyerezi – Mkuranga; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme Msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze – Segera na msongo wa Kilovoti 220 Segera – Tanga; 


- Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 220 kutoka Chalinze – Bagamoyo hadi Ununio Dar es salaam na ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli Shinyanga Kilovoti 400/220/33; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma (TAZA) na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma.


 Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Project) – Gridi Imara kwa kuendelea na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme pamoja na vituo vya kupoza umeme. 


- Serikali pia itaendelea kufanya matengenezo katika mitambo ya kuzalisha umeme, miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme pamoja na vituo vya kupoza umeme ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana wakati wote.  


Miradi ya Nishati Vijijini


-Mwaka 2024/25, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kuchukua hatua za kupeleka nishati vijijini ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii katika maeneo hayo. 


- Miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 20,000 ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ununuzi wa wakandarasi wa kutekeleza mradi, kufanya usanifu wa kina wa mradi na kuanza ujenzi wa miundombinu ya mradi. 


- Aidha, Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji katika Mkoa wa Songwe na Kigoma kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme Msongo Mdogo, kufunga transfoma na kuunganisha wateja. Vilevile, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 3,060 (vitongoji 15 kila Jimbo) kwa kujenga miundombinu ya mradi, kufunga transfoma na kuunganisha wateja. 


- Miradi mingine itakayotekelezwa ni mradi wa ujazilizi Awamu ya Pili B; mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili C; mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya Vijijini-Miji; mradi wa kusambaza umeme katika Migodi Midogo, maeneo ya Kilimo na Viwanda; mradi wa kupeleka umeme katika minara ya mawasiliano ya simu na mradi wa ufungaji wa mifumo ya umeme jua kwenye makazi yaliyopo Visiwani na yaliyopo mbali na Gridi ya Taifa.  


Nishati Safi ya Kupikia


- Katika mwaka 2024/25 Serikali itaendelea kutekeleza hatua madhubuti za kuimarisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia nchini. Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 – 2034 kwa kupatia ufumbuzi vikwazo vya matumizi ya nishati hiyo, ikiwemo gharama kubwa, upatikanaji hafifu na uhaba wa miundombinu yake na kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya nishati zisizo safi na salama za kupikia.


-Aidha, Wizara itaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya Nishati Safi ya Kupikia inayolenga Kuwawezesha Wanawake Barani Afrika Kutumia Nishati Safi ya Kupikia (African Women Clean Cooking Support Programme – AWCCSP. 


- Serikali pia itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza majiko banifu kwenye Kaya zilizopo katika maeneo ya Vijijini na Vijiji-Miji; kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa mkaa mbadala kwa ajili ya ununuzi wa mashine zitakazotumika katika uzalishaji wa mkaa huo.


-Kuendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza katika ujenzi wa miundombinu ya nishati ya kupikia katika maeneo 211 pamoja na kuendelea na usambazaji wa gesi asilia majumbani, hususan katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani.  


Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi



 -Serikali itaendelea kusimamia na kuendeleza Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi kwa kuchukua hatua mbalimbali, lengo likiwa ni kuhakikisha mchango wa Sekta hii katika maendeleo ya Taifa letu unaimarika. 


-Serikali itaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati na kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka kitalu cha Ruvuma (Ntorya) hadi Madimba lenye urefu wa kilomita 34.2 na uwezo wa kubeba futi za ujazo milioni 140 kwa siku.  


- Aidha, Serikali inatarajia kukamilisha majadiliano ya Mikataba ya mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia Kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG) ili utekelezaji wake uanze. 


-Serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa Gesi Asilia katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kufanya tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, usanifu wa kihandisi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwenye viwanda vya Mkuranga pamoja na Kongani ya Viwanda ya Kwala Mkoani Pwani. 


- Kukamilisha ujenzi wa vituo vya CNG (Kituo Mama katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Vituo vidogo vya Kairuki na Muhimbili) mkoani Dar es Salaam; na ununuzi wa vituo vitano (5) vya CNG vinavyohamishika (mobile CNG stations) vitakavyotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam.


-Aidha, Sekta Binafsi itaendelea kushiriki katika ujenzi wa vituo vya CNG pamoja na karakana za kubadilisha mifumo ya matumizi ya nishati ya gesi asilia (CNG) kwenye magari. 


- Vilevile, TPDC itakamilisha awamu ya kwanza ya mradi wa usambazaji wa gesi asilia chini ya ufadhili wa REA ambapo nyumba 980 zitaunganishwa katika mikoa ya Lindi na Pwani; na kuanza awamu ya pili ya mradi huo kwa kuendelea kusambaza gesi asilia maeneo ya Mkuranga, mkoani Pwani. 



- Miradi mingine itayakayotekelezwa ni mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima - Uganda hadi Tanga - Tanzania (East African Crude Oil Pipeline – EACOP); ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa Gesi Asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani na ujenzi wa miundombinu ya hifadhi ya kimkakati ya mafuta. 



- Serikali kupitia PURA inatarajia kuendesha Duru ya Tano (5) ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa lengo la kutangaza kwa wawekezaji vitalu vilivyo wazi katika eneo la bahari na nchi kavu. 


# Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni zitakazoongoza mnada wa vitalu, kufanya maonesho ya kitaalamu kuhusu vivutio vya vitalu na kuzindua Duru ya Tano (5) ya kunadi vitalu. Aidha, EWURA itaendelea kusimamia udhibiti wa huduma za nishati nchini kwa kuwasimamia watoa huduma kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora na uhakika. 


IMEANDALIWA NA OFISI YA NAIBU WAZIRI MKUU NA WIZARA YA NISHATI

Comments