CHANGAMOTO YA UHABA WA MAJI WATOWEKA SHULENI



 Waumini wa kanisa la Pentekost Galilaya Tanzania lenye makau makuu yake katika mji wa Runzewe limeguswa na adha ya maji inayowakabili wanafunzi wa shule ya sekondari Siloka halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani Geita baada ya kuvuta huduma ya maji safi na salama hadi shuleni hapo. 


Ilikuwa mapema ya February 13,mwaka huu waumini wa kanisa hilo walipokusanyika kwenye shule hiyo na kuchimba mtalo wa kupitisha bomba la maji hadi kuhakikisha maji hayo yanatoka katika shule hiyo.



Akizungumziahatua hiyo kwa niaba ya Askofu mkuu wa kanisa hilo nchini,Silvanus Fakomuha katibu mkuu wa kanisa hilo  Dominic Kulinganila alisema wao kama kanisa wameguswa na adha inayowakabili wanafunzi hao na hivyo kuamua kutoa huduma hiyo ikiwa ni sehemu ya kuisaidia jamii inayowazunguka.


“Sisis kanisa tumeamua kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassani na mbunge wetu ambaye ni naibu waziri mkuu na waziri wa nishati Mh.Dkt Doto Biteko katika juhudi za maendeleo kwa kutoa huduma katika jamiii inayotunguka”  alisema katibu Kulinganila.


Alisema, kanisa hilo limegharimia kuchimba mtalo wa kupitisha bomba na kununua vifaa vyote hadikuhakikisha maji yanatoka shuleni kwa gharama ya shilingi 700,000 ikiwa ni kuwaondolea adha wanafunzi ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda wa masoko kutafuta maji.


Pia,kanisa hilo limetoa miche 60 ya miti ya mbao na matunda kwa ajili ya kuboresha mazingira ya shule hiyo iliyoanzishwa mwaka jana kwa nguvu za wananchi na serikali.


Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Uyovu ilipo shule hiyo John Ditu alisema shule hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka jana haikuwa na huduma ya maji na kwamba wanafunzi walikuwa wanahangaika kupata hiyo hiyo kwenye visima na kwa majira na wakati mwingine walikuwa wanakosa maji.


Alisema, maji hayo hayakuwa salama na kwamba baadhi ya wanafunzi walikuwa wanaugua matumbo mara kwa mara kutokana na kutumia maji yasiyokuwa safi na salama kwa kunywa na kupikia.


Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo Khadija Mussa na Maxmillian Wilson walisema, shule hiyo ilikuwa na ukosefu wa maji kwa muda mrefu  na hivyo walilazimika kutumia zaidi ya nusu saa kila siku kutafuta maji na hivyo baadhi ya vipindi walikuwa wanachelewa kuanza.


“Huduma ya maji ilikuwa inatusumbua sana katika kusoma kwani wanafunzi wakija wanatafuta maji na kuanza kufanya usafi darasani,na maji tuliyokuwa tunatumia hayakuwa safi na salama,na maji yale yalikuwa sio safi na salama kwa matumizi ya kunywa au kupikia”  alisema Khadija.


Mkuu wa shule hiyo Gisela Amani amelipongeza kanisa hilo kwa kuwasaidia wanafunzi na jumuiya ya shule kwa ujumla kwa kutoa msaada huo wa maji kwani moja ya changamoto zinazowasumbua wanafunzi katika masomo ni pamoja ukosefu wa maji.


Alisema, ili wanafunzi waweze kufanikiwa vizuri katika masomo ni muhimu kuwa na huduma ya maji safi na salama ambayo itawatoa katika msongo wa kufikiria kutafuta maji na badala yake kujikita kusoma.


“Ni jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa huduma hii,elimu bora haishi darasani ,ili elimu bora ipatikane lazima kuna mambo kama haya ya maji ,tunawashukuru sana waumini hawa kwa kutuletea maji ,hivyo sisi uongozi wa shule na wanafunzi tunashukuru sana waumini,viongozi wa serikali kuhakikisha tunapata elimu bora” alisema Amani.


MWISHO

Comments